November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Atuhumiwa kwa mauaji ya mke wake kwa madai ya kuambukizwa ugonjwa

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavi.

JESHI la Polisi Mkoa wa Katavi limefanikiwa kukamata na kuwashikiria watu 12 kwa tuhuma za kufanya matukio ya mauaji katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo ambapo miongoni mwao ni mtuhumiwa wa mauaji ya mke wake.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, SACP Kaster Ngonyani akitoa taarifa Julai 05, 2024 ofisini kwake mbele ya waandishi wa habari ameeleza kuwa jeshi hilo haliwezi kuruhusu watu wenye nia ovu kutoa uhai wa watu wengine kinyume cha sheria.

SACP Kaster akifafanua tukio la mauaji ya mwanamke mmoja kuuliwa na mume wake kwa njia ya kukatwa katwa na mapanga sehemu zake za mwili kwa madai ya kuambukizwa ugonjwa (ugonjwa umehifadhiwa) mtuhumiwa huyo amekamatwa.

Amesema “Tumemkamata pamoja na watuhumiwa wengine wa mauaji waliyoyafanya kwa nyakati tofauti na mara baada ya taratibu za kisheria kukamilika kukamilika watafikishwa mahakamani”

“Mtu amemuhisi mke wake kumletea ugonjwa nyumbani kwake kwahiyo kaamua kumuuwa mke wake na yeye mwenyewe akaamua kunywa sumu lakini hajafariki na yeye mwenyewe amekiri kutenda kosa hilo,”Amesema SACP.

Kamanda huyo wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi amesema chanzo cha mauaji mengine ni wivu wa mapenzi,Imani za kishirikina na visasi kati ya mtu na mtu ambapo aliweza kutoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi.

SACP Kaster amesema watuhumiwa wengine 30 wamekamatwa kwa makosa ya unyang’ang’anyi, uporaji hasa wa nyakati za usiku na wamekutwa wakiwa na mali zidhaniwazo kuwa za wizi ambazo ni Runiga 7,vipande vya nondo,pikipiki yenye usajili MC. 118 DLT aina Star,,vipande vya vitasa vya milango,vifaa vya baskeli,bomba za maji,vifaa vya pikipiki,loki za madirisha na madirisha ya aluminium.

Vilevile watuhumiwa 24 wamekamatwa wakiwa na pombe ya moshi kiasi cha lita 251, watuhumiwa 7 wakiwa na dawa za kulevya aina ya bangi debe moja na kete 287 humu mwingine mmoja akiwa na silaha haramu aina ya gobore ikiwa na risasi mbili.

Kwa kipindi cha mwezi Juni, 2024 amesema jumla ya makosa 2853 ya usalama barabarani yamekamatwa na kutozwa faini ambapo ni sehemu ya mafanikio ambayo jeshi hilo limepata ya utendaji kazi.

Mafanikio mengine katika kesi walizoziwasilisha mahakamani jumla ya watuhumiwa 21 walipatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo mbalimbali.

Jeshi la Polisi mkoa wa Katavi limetoa rai kwa wananchi kuacha vitendo vya kialifu pamoja na kutokuacha kutoa taarifa za uhalifu zinapotokea huku wanunuzi wa vyuma chakavu wajiepushe kununua mali za wizi.