December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Attar Neyshabouri Malenga wa Kiiran

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Tarehe 25 Farvardin kwa mujibu wa ( Kalenda ya Kiirani) inayosadifiana na tarehe 14 Aprili, ni siku ya kumkumbuka na kumuadhimisha malenga wa Kiirani Farid al-Din Abu Hamid Muhammad bin Abu Bakr Ibrahim bin Is- haq Attar Neyshabouri, ambaye ni mmoja wa washairi mashuhuri, aaref na mwanafikra mkubwa wa Kiirani aliyeishi mwishoni mwa karne ya sita na mwanzoni mwa karne ya saba Hijria. Baadhi ya wanahistoria wameandika kuwa, mwanafikra na malenga huyo wa Kiajemi amezaliwa mwaka 513 na wengine wanaeleza kuwa alizaliwa mwaka 537 Hijiria.

Attar Neyshabouri alizaliwa katika kijiji cha Kadkan au Shadiakh, ambacho wakati huo kilikuwa sehemu ya jiji la Neyshabour. Hakuna habari inayoelezea taarifa zake za utotoni mwake, isipokuwa baba yake aliishi katika mji wa Shadiakh akifanya kazi ya kuuza dawa za asili, na alikuwa mahiri na hodari mno katika biashara hii ya kuuza dawa za asili, na baada ya kufariki dunia baba yake, Farid al Din Attar Neyshabouri aliendeleza shughuli za marehemu baba yake ya kuuza dawa za asili.

Wakati akishughulika na uuzaji wa dawa za asili Attar Neyshabouri alikuwa akitoa tiba ya asili na wala haijulikani utaalamu huo wa kutoa tiba ya asilii aliupata kutoka kwa nani.

Attar Neyshabouri aliendelea na shughuli zake za kutoa tiba ya asili sanjari na kuuza dawa za asili hadi pale yalipopatikana mapinduzi ya kiroho na kimaanawi kwa upande wake, na jambo hili limebainishwa kwa kutolewa visa kadhaa, lakini kisa maarufu ni hiki kifuatacho:
Siku moja Attar Neyshabouri alikuwa dukani kwake akifanya shughuli zake, mara akaingia Darwesh” na akaanza kusema maneno kadhaa yanayohusiana na Mwenyezi Mungu, ili Attar aweze kuvutika na kumsaidia, lakini Darwesh hakupata msaada wowote kutoka kwa Attar Neyshabouri.

Darwesh akamwambia Attar : Ewe kijana unataka ufariki duniani kwa kifo cha namna gani? Attar akajibu: Kwa njia ileile ambayo wewe unataka kufa. Darwesh akasema; Wewe unataka kufa kama nitakavyokufa mimi? Attar akajibu: Ndio, Darwesh akachukua bakuli lake lililotengenezwa kwa mbao na kuliweka chini ya kichwa chake na akasema maneno ya Mwenyezi Mungu na hatimaye kufariki dunia. Kwa vile Attar Neyshabouri aliliona tukio hilo kwa macho yake aliathirika mno na kubadilika na akaamua kutoka dukani na kubadilisha kikamilifu mtindo na mwenendo wa maisha yake .

Attar Neyshabouri aliposhuhudia tukio hilo la Darwesh , akaacha kabisa shughuli za tiba na biashara za dawa za asili, na akaamua kuelekea kwa Sheikh Mkuu Aref Rukniddin Akaf , wakati huo Sheikh Aref alikuwa mtu maarufu na mashuhuri mno na kwa miaka kadhaa Attar Neyshabouri alikuwa akipata elimu na maarifa kutoka kwa sheikh Aref Rukniddin Akaf.

Attaf Neyshabouri aliweza kutumia nusu ya umri wake kwa kufanya safari katika miji mbalimbali, na katika safari zake hizo alifanikiwa kukutana na masheikh wakubwa wakubwa katika zama hizo, na safari hizo ziliweza kumfikisha hadi kwa sheikh Majiduddin Baghdadi.

Inasemekana kuwa Sheikh Aref alipofikia marika ya uzee, Bahauddin Muhammad baba wa Jalaluddin Balkhi alikuwa pamoja na mwanawe walifanya safari ya kuelekea Iraq , wakiwa njiani walipitia Neyshabouri na wakafanikiwa kumtembelea Attar Neyshabouri, hivyo Sheikh Attar Neyshabouri alitoa nakala moja kati ya makala zake za mashairi na kumpa Jalaluddin ambapo wakati huo alikuwa bado kijana mdogo mno.

Sheikh Attar Neyshabouri alikuwa ni mchapakazi na mwenye harakati kubwa, iwe wakati ule alipokuwa akijishughulisha na shughuli za utabibu na uuzaji wa dawa za asili au katika kipindi cha uzee akiwa akijishughulisha na uimbaji na uandishi wa mashairi na nathari.

Kauli mbalimbali zimetolewa kuhusiana na kifo chake na baadhi ya wanahistoria wameeleza kuwa, Sheikh Attar Neyshabouri alifariki dunia mwaka 627 Hijria na baadhi ya wengineo wanasema kuwa, Sheikh Attar alifariki mwaka 632 Hijria, lakini kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa, wanahistoria wengi wanasema kuwa Sheikh Attar Neyshabouri alifariki dunia mwaka 627 Hijria
Wanahistoria hao wanaelezea kuwa, kifo chake kilitokea zama za Wamogholi walipouvamia mji wa Neyshabouri na mmoja kati ya askari vamizi wa Kimogholi alimuuwa Sheikh Attar Neyshabouri.

Sheikh Bahauddin ameelezea kisa na tukio la kifo cha Sheikh Attar kwenye kitabu chake mashuhuri kinachoitwa Koshkuul.

Sehemu ya kitabu hicho imeandikwa kuwa, wakati askari wa Kimogholi walipovamia mji wa Neyshabouri, waliwauwa kwa halaiki wenyeji wa mji huo, askari hao vamizi walifanya vitendo vya kinyama dhidi ya wakaazi wa Neyshabouri, na askari mmoja wa Kimogholi alimpiga upanga Sheikh Attar Neyshabouri uliosababisha kifo chake.

Kwa vile damu nyingi ilimwagika kutoka katika majeraha yake, hivyo kabla ya kufariki dunia Sheikh Attar aliandika kwa kutumia damu yake iliyokuwa ikichuruzika mwilini kwenye ukuta masaibu yaliyomkuta, na yaliyopelekea kufariki kwake dunia.

Kaburi la Sheikh Attar liko karibu na mji wa Neyshabour, kaburi hilo liliwahi kuharibiwa katika zama za Teimuriyan, na kukarabatiwa tena kwa amri ya Amir Alishir Navai, Waziri wa Sultan Hussein Bayqara.

Athari za kazi za Malenga Sheikh Attar Neyshabouri zimegawanyika katika makundi mawili: Ushairi na Nathari. Kazi zake za ushairi ni kama vile, mkusanyiko wa mashairi na kaswida. Kazi zake za Nathari ni kama vile Asraar Nameh, Elahi Name, Musibat Nameh, Bolbol Nameh na nyinginezo.

Malenga Attar Neyshabouri ni mmoja wa washairi wakubwa na mmoja wa watu mashuhuri katika historia ya fasihi ya Kiirani. Maneno yake ni rahisi, ya kuvutia na yenye kutoa mguso maalumu.

Sheikh Attar alikuwa akichagua njia bora ya kuelezea mashairi yake yaliyokuwa ya kiirfani, njia ambayo ni kuleta maneno rahisi na yasiyoathiriwa na maneno mengine. Ingawa kidhahiri hakuwa na maneno na maelezo yenye wigo mpana zaidi na wenye uimara kama ule wa Sanai, lakini maneno yake hayohayo mepesi yalikuwa yakichoma nyoyo za watu na kupelekea kuwa mwimbaji mwenye mvuto mkubwa.

Hali kadhalika msaada aliokuwa akiupata kutoka katika visa na hekaya mbalimbali, ni mojawapo ya mvuto wa athari zake na kuwa chimbuko la kiirfani baada yake kama vile akina Moulavi na Jami, kwani shakhsia hao wawili walikuwa wasomaji wakubwa na wazuri wa nathari na kaswida.