November 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dkt. Fredrick Shoo

Askofu Shoo afunguka vita dhidi ya Corona

Na Mwandishi Wetu, Moshi

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dkt.
Fredrick Shoo amewataka wananchi kuchukua tahadhari zote na kufuata
maelekezo yanayoelekezwa na Serikali juu ya kujilinda dhidi ya
maambukizi ya virusi vya Corona.

Askofu Dkt. Shoo alitoa wito huo jana wakati akihubiri kwenye ibada ya
Pasaka katika usharika wa Moshi mjini.Alisema na kila mmoja ana wajibu
wa kujilinda na kuwalinda wengine dhidi ya ugonjwa huo.

Alitumia ibada hiyo kuwata wananchi kumgeukia na kumtegemea Mungu
katika kipindi hiki kigumu cha janga la Corona, kwa kuwa kwa akili,
nguvu na uwezo wa binadamu wenyewe havitaweza kupambana na janga hilo.

Aliongeza kwamba huu ni wakati wa kila mmoja kuomba na kumuita Mungu
ili aweze kuliondosha janga la Corona. “Tuchukue tahadhari zote na
kufuata maelekezo yote, lakini tusiache kumtazama huyu Yesu aliye na
nguvu na tumaini letu lililo kuu kuliko yote.

Tumuombe sasa huyu Yesu mfufuka, aturejeshee tena amani, tumaini,
atupe uhai na kutukingia hatari zote, hata janga hili la Corona,
ambalo limeleta hofu na huzuni duniani,” alisema Dkt. Shoo.

“Yesu kristo anasema tusiogope. Wapendwa neno hili likawe ujumbe mkuu
wa Pasaka na nguvu yetu, gonjwa hili linatisha, watu wamejawa hofu
sana, lakini hofu yetu isitupe kutaharuki na kukosa amani ya ndani
bali amani yetu ikawe ni tunaye Yesu mfufuka, ambaye ni nuweza wa
yote,” alisema na kuongeza;

“Tutoke hapa tukiwaambia watu Corona ipo tujihadhari lakini Yesu
Kristo yupo, ambaye ni mshindi wa kifo na mauti, tuendelee kumuomba na
kumuita Mungu maana yeye mwenyewe aliahidi, tukimuita ataitika na
kutuonyesha mambo makubwa na magumu tusiyoyajua.”

Alisema iwapo wananchi wote wakiungana pamoja kuchukua tahadhari  na
kuzingatia maagizo yanayotolewa katika kuzuia virusi vya Corona kuenea
na kuomba kwa pamoja Mungu atasikia na kuiponya nchi.