Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Leo tarehe 29/12/2012 viongozi mbalimbali, ndugu, jamaa na marafiki wamehudhuria katika ibada ya kuuaga mwili wa Askofu Mkuu Msataafu Ranwell Mwanisongole wa kanisa la TAG ambapo ibada ya kumuaga imefanyika katika kanisa la City Christian Church (CCC) Upanga jijini Dar es Salaam.
Mwili wa Askofu Mwenisongole baada ya kuagwa leo umesafirishwa Mkoani Songwe kwaajili ya Mazishi ambayo yatafanyika kesho tarehe 30/12/2021,.
Ranwell Marko Mwanjonde Mwenisongole alizaliwa tarehe 23 Julai 1946 katika Kijiji Cha Ichenjezya, Vwawa, Wilayani Mbozi
Ranwell alisoma elimu ya msingi katika shule ya Vwawa Middle School ambalo alifaulu na kujiunga na shule ya sekondari ya Malangali huko Iringa kuanzia mwaka 1964 na kuhitimu kidato Cha nne mwaka 1967.
Mwaka 1968, Ranwell alichaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari ya juu katika Tajnisi ya Sayansi ya fizikia, Chemia na Hisabati (PCM) lakini alibadilisha akasoma Tajnisi ya Biashara yaani ECA huko karimjee School ambayo kwa sasa inaitwa Usangara High School.
Mwaka 1969 Ranwell alichaguliwa kujiunga na Mafunzo ya jeshi la kujenga Taifa (JKT) huko Masange, Tabora Kwa mujibu wa sheria katika ‘Operation Mikoa’ na baadaye alihamishiwa Kambi ya Ruvu JKT ambako alimalizia mafunzo yake.
Septemba mwaka 1970 Ranwell alijiunga na Masomo ya Shahada ya biashara katika chuo kikuu Cha Nairobi, Kenya akiwa sehemu ya wanafunzi 14 wa kitanzania waliojiunga na chuo hicho.
Mwaka 1972 Ranwell alihitimu masomo yake na kurejea nyumbani ambako alipangiwa kazi katika Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na alifanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kupanda cheo mpaka kufikia cheo Cha Meneja Mkuu
Kuhusu Maisha ya Ndoa na Familia, Desemba 16, 1973 Ranwell alifunga ndoa na Irene Mbona katika kanisa la Vwawa Moravian na wakajaliwa watoto wanne wakiume, wajukuu wanne ambapo wakiume watatu na wakike mmoja.
Mbali na hayo Askofu aliokoka na alianza kutoa huduma za kiroho ambapo Mwaka 1982 Ranwell aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa Taifa wa Idara ya Elimu ya kikristo wa TAG, huduma aliyoifanya kwa miaka mingi
Pia kuhusu huduma ya Kitaifa na kimataifa, Mwaka 1992 Ranwell alichaguliwa kuwa Askofu Mkuu wa Tanzania Assemblies of God jukumu alilohudumia kwa miaka 16 mfululizo mpaka mwaka 2008 .
Aidha kuhusu ujenzi wa CCC, Mwaka 1989 Askofu Mwenisongole aliliongoza kanisa la CCC Upanga kuanza mradi wa ujenzi wa kanisa katika kiwanja kilichokuqa kimepatikana karibu na Kona ya mtaa wa Olympio na Bibi Titi Street Upanga
Agost 2000 Askofu Mwenisongole alianzisha ujenzi wa kanisa la CCC Upanga ambapo kanisa lilipo sasa.
Desemba 2002 miaka 20 kamili iliyopita Askofu Mwenisongole aliendesha ibada ya Christmas katika jengo la kanisa ambalo lilikuwa halijakamilika vizuri na Novemba 1, 2009 Ukumbi wa Kanisa ulifunguliwa rasmi kwa ajili ya matumizi ya Ibada .
Kuhusu mafanikio ya huduma, Askofu Mwenisongole alikuwa ni mhubiri na mwalimu mzuri anayefundisha kweli yote ya Neno. Alikuwa mlezi wa Vipawa vya vijana na watumishi wa chini ya huduma yake wanafunzi wengi wa shule na vyuo walikuwa washiriki na kulelewa.
Askofu Mwenisongole amezaa zaidi ya wachungaji 28 walioko Tanzania na nchi zingine Duniani na amekuwa ni kiongozi katika nyadhifa mbalimbali kitaifa, Afrika na Ulimwenguni.
Amekuwa Askofu Mkuu wa TAG kwa miaka 16, Mjumbe wa Assemblies of God Global Committee na Makamu wa Rais wa African Association of Assemblies of God kwa miaka kadhaa.
Amehuburi jumbe zaidi ya 4500 hapa Tanzania, Singapore, South Korea, Marekani na nchi zingine.
Kuhusu Nishani na Tunu mbalimbali, Askofu Mwenisongole alitunukiwa tuzo na Tunu mbalimbali na watu binafsi mashuhuri, vyuo na Taasisi mbalimbali kwa uongozi na utumishi wake ndani na nje ya nchi.
Mwaka 2012 Askofu Mwenisongole alitunukiwa Shahada ya juu ya heshima ya Uzamifu katika uongozi wa kanisa (Honorary doctorate of church leadership)
Mwaka 2014 katika sherehe za miaka 75 ya TAG, Askofu Mwenisongole alitunukiwa Nishani ya juu ya uongozi wa kanisa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete.
Tarehe 4 May 2019 Askofu Ranwell Mwenisongole alitunukiwa u Professor wa Phalsafa katika uongozi na Omega Global University.
Askofu Ranwell Mwenisongole alimaliza safari yake tarehe 25/12/2021 saa 11:00 alfajiri kwa ushindi akiwa amezungukwa na mkewe na wanafamilia baada ya kujisikia vibaya kidogo.
Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Jina la Bwana lihimidiwe.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua