January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Askofu Mwakipesile: Tuendelee kutunza amani iliyopo nchini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Dkt. Brown Abel Mwakipesile ameiasa jamii kudumisha amani na utulivu uliopo nchini ili kuendelea kuwa na uhuru wa kuabudu na kushiriki katika maendeleo ya Taifa ka ujumla.

Ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya Uwekaji jiwe la msingi katika ujenzi wa Chuo cha Biblia pamoja na uzinduzi wa Ofisi Kuu ya Kanisa hilo zilizopo eneo la Ilazo Jijini Dodoma.Halfa hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Kamati kuu ya kanisa hilo, Maaskofu kutoka nje ya nchi ikiwemo;Malawi, Zambia na Rwanda, Maaskofu wa Kanda, Majimbo pamoja na wachungaji wa kansa hilo.

Alisema kuwa, wataendelea kuiombea nchi huku akitoa rai kwa jamii kuendelea kutunza amani iliyopo kwa kuzingatia uwepo wa amani ndiyo chanzo cha maendeleo ya watu na taifa.

“Ni jukumu letu kuendelee kuiombea nchi yetu ili amani iliyopo idumu na kusaidia watu kuendelea kuabudu kwa uhuru na kushiriki katika shughuli za ujenzi wa Taifa kwa utulivu, alisema,” Dkt. Mwakipesile

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kogwa Mhe. Remidius Mwema kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka alisema Serikali inaunga mkono jitihada zinazofanywa na makanisa ikiwemo la EAGT huku akipongeza hatua ya ujenzi wa Chuo pamoja na Uzinduzi wa jengo la Ofisi Kuu la Kanisa hilo na kuwaomba wananchi kuendelea kuiombea nchi huku akiwasihi vijana kuifanya kazi ya Mungu kwa bidii kwa kuzingatia ni kundi muhimu na linalotegemewa katika maendeleo yaTaifa

“Vijana tumeandikiwa kuwa wenye nguvu hivyo ni vyema kuzitumia nguvu katika kumtumikia Mungu kwenye kila nafasi ambayo Mungu amekuheshimu na kukuweka, tuendelee kufanya kazi kwa bidii na kujiletea maendeleo yetu,”

Aidha alipongeza umoja na mshikamano wa kanisa la EAGT ambalo limeweza kujenga majengo hayo kwa vyanzo vyao vya mapato kwa kuhakikisha kila mshirika anashiriki katika masuala yanayohusu maendeleo yao.

Sambamba na hilo, alitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi wote kushiriki katika sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kuanza tarehe 28 Agusti, 2022.

Akitoa taarifa ya mipango ya Kanisa, Mkurugenzi wa Mipango na Miradi Mchungaji Profesa Frugence Binagwa alisema kazi ya ujenzi ilihusisha juhudi za waumini kuanzia ngazi ya makanisa ya mahali pamoja ambapo kila mshirika huchangia zoezi hilo.

“Fedha ya ujenzi zimetokana na utaratibu uliopitishwa na Kanisa kwa kila Mshirika kutoa sadaka ya sh. 200 kwa wiki na Mchungaji sh 1000 kwa wiki. Hivi sasa Kanisa limeweza kukusanya milioni 425, ambazo sehemu yake imejenga Ofisi hii na Ujenzi wa Chuo cha Biblia unaoendelea”alisema Profesa.

“Ujenzi wa Ofisi za kutoa huduma kwa Watanzania ni lengo namba 15 ni kati ya Malengo mahsusi 20, Linalotimiza azma ya Kanisa la EAGT kuwa na Makao Makuu yake Dodoma baada ya Makao Makuu ya Nchi kuhamia Dodoma na EAGT imeamua kufanya. Ujenzi huu wa Ofisi za Makao makuu ya EAGT ulipitishwa na Baraza la waangalizi kama sehemu ya utekelezaji Julai 2022”.alisisitiza Profesa Binangwa

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CPCT Askofu Peter Nkonki alipongeza jitihada za uongozi wa kanisa hilo kwa kuendelea kushikamana na kufikia malengo ya ujenzi wa Ofisi Kuu na Chuo Kikuu cha Biblia cha Kanisa hilo huku akiahidi kuendelea kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali ikiwa  ni ishara ya kuunga mkono juhudi za maendeleo ya kanisa hilo.

AWALI

Kanisa la EAGT lilisajiliwa rasmi tarehe 18, Julai 1991 kwa usajili Na. SO. 7183, Chini ya usimamizi wa aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Dkt. Moses Kulola Kanisa lina makanisa ya mahali pamoja zaidi ya 5000 yaliyo katika Kanda 13 na Majimbo 93 Kanisa ina mpango mkakati wa miaka mitano ambapo Dira ya Mpango Mkakati huo uliothibisha maono ya EAGT kuwa ni; “Habari njema ya wokovu imewafikia watu wote nchini Tanzania na Nje ya Nchi”. Hii ni katika kutekeleza agizo Kuu la Yesu Kristo. 

Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Dkt. Brown Abel Mwakipesile akifungua kitambaa kuashiria uzinduzi rasmi wa Ujenzi wa Jengo la Chuo Kikuu cha Biblia (ECBC) cha kanisa hilo kilichopo Ilazo Jijini Dodoma, kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kogwa Mhe. Remidius Mwema kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka
Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Dkt. Brown Abel Mwakipesile pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kogwa Mhe. Remidius Mwema wakifurahia mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo Kikuu cha Biblia (ECBC) kilichopo Ilazo Jijini Dodoma
Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Dkt. Brown Abel Mwakipesile akizungumza kabla ya uzinduzi rasmi wa Jengo la Ofisi ya Kanisa hilo lililopo Ilazo Jijini Dodoma, hafla iliyohudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Maaskofu wa Kanda, Majimbo pamoja na Wachungaji.
Mshereheshaji (MC) Bw. John Mwangata (Mwangata the great) akisoma maandishi ya kwenye jiwe la msingi mara baada ya uzinduzi wa Jengo la Ofisi ya kanisa la EAGT zilizozinduliwa na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo.Kulia ni Dkt. Brown Abel Mwakipesile
Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Dkt. Brown Abel Mwakipesile akizungumza na viongozi mbalimbali wa Serikali na kanisa mara baada ya kukagua na kujionea ofisi mpya ya Kanisa hilo, iliyojengwa eneo la Ilazo Jijini Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kogwa Mhe. Remidius Mwema kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka akitoa salamu za mkoa katika hafla hiyo.
Mwenyekiti wa CPCT Askofu Peter Nkonki akizungumza wakati wa halfa hiyo.
Kwaya  ya  Utemini kutoka Singida ikiimba wimbo maalum wakati wa uzinduzi huo.
Kwaya Kuu ya Kanisa la EAGT Mlimwa West (New Jerusalem) ikiimba wimbo maalum wakati wa uzinduzi huo.
Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Dkt. Brown Abel Mwakipesile pamoja na meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Maaskofu waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Ofisi za Kanisa hilo pamoja na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kanisa hilo Jijini Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kogwa Mhe. Remidius Mwema akiweka saini kitabu cha wageni katika ofisi ya Kanisa la EAGT mara baada ya uzinduzi rasmi wa ofisi hiyo Jijini Dodoma.