Na Joyce Kasiki, Dodoma
ASKOFU wa Kanisa la Maombezi (EHC) Eliah Mauza, ameishauri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhakikisha dawa za tiba mbadala zitakazotumika katika mapambano ya Corona kuthibitishwa na mamlaka husika ili kuondoa wimbi la watu wengi kuibuka na kila mmoja kudai ana dawa ya kukabiliana na ugonjwa huo kwa njia ya kujifukiza.
Ushauri huo wa Askofu Mauza umekuja huku wananchi wengi wakionekana kutumia picha kweye mitandao ya kijamii wakijifukiza dawa, wakati dawa wanazotumia zikiwa hazijathibitishwa kama zina matokeo chanya katika vita hiyo.
Pia baadhi ya watumiaji wa dawa hizo za kujifukiza haijulikane kama wamepimwa na kuthibitika kama wamepata maambukizi ya virusi vya Corona au dawa hizo wanazotumia kama kinga.
Akizungumza jana jijini Dodoma Askofu Mauza alipongeza ushauri wa Rais Magufuli kuhusu tiba asili na kuunga mkono kauli yake ya kukataa kuwafungia wananchi ndani, kwani kufanya hivyo hilo ni janga kubwa kuliko Corona yenyewe.
Askofu Mauza alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya isiruhusu watu kutumia dawa holela kujitibu na Corona, kwani hatua hiyo inaweza kusababisha madhara zaidi.
“Kama alivyosema Rais Magufuli Wizara ya Afya isaidie hili. Itumie utaratibu wa kisayansi kukagua dawa wanazotumia kwenye tiba mbadala, kwani sio kila dawa inayotumika inaweza kutibu Corona,” alisema Askofu Mauza na kuongeza;
“Wizara iwaite watu wa tiba mbadala ili ikae nao na kuangalia kama dawa zao zinafaa kwenye tiba dhidi ya Corona.
Vinginevyo kila mmoja anaanza kutangaza kwamba ana dawa ya Corona…kwa hiyo hili suala liwekwe vizuri, Rais ametangaza kutumika kwa tiba asili lakini ni vyema Wizara ya Afya isiliache jambo hili.”
Alisisitiza kwamba ni muhimu dawa wanazotumia wananchi kujifukukiza zithibitishwe na maabara za kisayansi, bila hivyo Taifa litaenda pabaya.
“Tukumbuke ya Mzee wa Samunge (kikombe cha babu), alipoanza kutibu magonjwa mbalimbali,watu wengi walikimbilia huko na wengi walikufa licha ya kunywa kikombe hicho kwa sh. 500 tu. Kama hatutakuwa makini watu wataacha kwenda hospitali watakimbilia kwa waganga.”
Kuhusu kuwafungia Watanzania ndani, Askofu huyo alisema kikubwa kinachohitajika ni tahadhari. “Lockdown sioni kama dawa. Dawa ni maombi maana kesi huwa zinaisha kwa ushahidi maana katika Biblia Daud aliomba na ugonjwa wa tauni ukaondoka,”alisema.
Aliendelea kushauri maombi ya kitaifa kama ambayo yalihudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yashuke chini kuanzia kwenye mikoa, wilaya hadi vijiji ili kuweka nguvu kubwa kwa Mungu katika kupambana na Corona.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria