Na Stephano Mango,Timesmajira Online. Songea
WAKAZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wametakiwa kuendelea kuthamini uwepo wa vyoo bora katika makazi yao, ili kuondokana na uwezekano wa magonjwa ya mlipuko.
Wito huo umetolewa jana na Ofisa Afya Halmashauri ya Wilaya ya Songea, John Kapitingana wakati akizungumza na Majira ambapo alisema asilimia 87 ya wakazi wa halmashauri hiyo wanavyoo bora vyenye sifa na uwezo wa kupambana na magonjwa.
Kapitinga amezitaja sifa za vyoo bora kuwa ni vyenye milango, sakafu inayoweza kusafishika vizuri, vinavyotunza faragha kwa mtumiaji pamoja na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza.
Ofisa huyo amesisitiza kwamba kupitia ‘Kampeni ya nyumba ni Choo’, halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa afya imefanikiwa kwa asilimia 87 kuhamasisha jamii kujenga vyoo bora ambavyo vinakubalika kwa matumizi ya kibinadamu.
Kampeni ya nyumba ni choo ni elimu inayotolewa kwa wakazi wote nchini, ili kuhakikisha wananchi wanajenga na kutumia vyoo bora badala ya kujisaidia ovyo na kusababisha kuenea kwa magonjwa ya kuhara, kipindupindu, kichocho cha tumbo na magonjwa ya milipuko ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kijiji cha Parangu, Patriki Komba amesema wanashukuru wadau wa afya kwa kuanzisha kampeni hiyo, ambayo imewasaidia kupata uelewa kuhusa umuhimu wa kutumia vyoo bora katika makazi yao.
Amesema katika Kijiji hicho, asilimia kubwa ya wakazi wamejitahidi kujenga vyoo bora na maeneo ya kutakasa mikono baada ya kutoka chooni na kutengeneza vichanja kwa ajili ya kuanikia vyombo na usalama wake.
Ametoa wito kwa wadau wa afya, kuendelea na kampeni ya nyumba ni choo kwa lengo la kuzifikia kaya zote kwa asilimia mia moja ifikapo Julai 2022.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi