March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asilimia 87 wanafunzi wa kidato cha kwanza Ilemela wameripoti shuleni 

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imesema kuwa hadi Februari 5, 2026, jumla ya wanafunzi 9,897 wa kidato cha kwanza sawa na asilimia 87 wamekwisha ripoti shuleni kati ya wanafunzi 11,348 waliopangiwa kujiunga  kwa mwaka wa masomo 2026.

Akizungumza na Timesmajira Online Februari 6,2026, Ofisa Elimu Maalumu Sekondari wa Halmashauri  ya Manispaa ya Ilemela, Mwalimu Mugyabuso Witness, amesema kati ya wanafunzi waliopangiwa kujiunga na kidato cha kwanza  katika Halmashauri hiyo wavulana ni 5,474 na wasichana 5,874. Kati ya walioripoti, wavulana ni 4,785 huku wasichana wakiwa 5,112.

Amesema mwitikio ni mzuri ikizingatiwa kuwa ni wiki ya tatu tangu shule kufunguliwa kwa muhula mpya wa masomo wa mwaka 2026.

“Mwitikio ni mzuri,ni wiki ya tatu tangu shule kufunguliwa na tayari tumefikia asilimia 87 ya wanafunzi walioripoti. Tunaamini kufikia mwishoni mwa Februari tutafikia asilimia 100,” amesema Mwalimu Mugyabuso.

Amesema,Halmashauri  hiyo ina jumla ya shule za sekondari 62, kati ya hizo 37 ni za Serikali na 25 ni za binafsi.

Mwalimu Mugyabuso,amesema Halmashauri inatumia viongozi wa mitaa, kata pamoja na wanafunzi waliokwisha ripoti kama mabalozi wa kuhamasisha wenzao ambao bado hawajaripoti shuleni.

“Tunatumia wanafunzi waliokwisha fika shuleni kuulizana mitaani, wakisema mwanafunzi fulani amepelekwa shule binafsi tunaomba waje kutoa taarifa rasmi,” amesema.

Ameongeza kuwa Halmashauri imewaruhusu wanafunzi kuanza masomo hata kama hawajakamilisha mahitaji yote ikiwemo sare za shule, huku wazazi wakiendelea kufanya jitihada za upatikanaji wake.

Pia amesema changamoto iliyopo ni baadhi ya wazazi kuwapeleka watoto wao shule za binafsi bila kutoa taarifa kwa shule walizopangiwa awali, hali inayosababisha ucheleweshaji wa takwimu sahihi.

“Kuna wanafunzi 1,134 waliokwenda shule binafsi, lakini bado kuna idadi kubwa ambayo taarifa zao hatujazipata. Hii inatupa mwanya katika ufuatiliaji,” amesema.

Amesisitiza kuwa hadi sasa Halmashauri haijakumbana na changamoto ya wanafunzi kushindwa kuripoti shule kutokana na mimba.

Hali ya kuripoti wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule mbalimbali ndani ya Halmashauri hiyo,amesema zipo baadhi ambazo zimeripotiwa kuwa na mwitikio mdogo wa uripoti ikiwemoa shule ya sekondari Nyasaka ambayo imepangiwa wanafunzi 664, lakini hadi Februari 5, 2026 walioripoti ni asilimia 62.

Shule ya Sekondari Shibula imepangiwa wanafunzi 351, ambapo asilimia 68 wameripoti huku asilimia 32 wakiwa bado hawajafika. Sekondari Lubuka iliopo Kata ya Kahama imepangiwa wanafunzi 321, ambapo asilimia 51 wameripoti.

Sekondari Angeline Mabula imepangiwa wanafunzi 362, kati yao 239 sawa na asilimia 66 wamekwisha ripoti huku asilimia 34 bado hawajaripoti.

Kwa upande wa shule zenye mwitikio mzuri ni pamoja na sekondari ya Ibungiro iliyopangiwa wanafunzi 414, ambapo 413 sawa na asilimia 99.9 wameripoti huku mmoja akiwa bado hajaripoti.

Shule ya sekondari Lumala, imepangiwa wanafunzi 351, walioripoti mpaka sasa ni sawa na asilimia 100 huku sekondari Nundu imepangiwa wanafunzi 412 na wote wameisha ripoti sawa na asilimia 100.

Shule nyingine ni sekondari Nyamanoro ambayo imepangiwa wanafunzi 296 kati yao wavulana 139 na wasichana 157na wote wameisha ripoti sawa na asilimia 100.

Pasiansi sekondari wanafunzi 261 na wote wameripoti sawa na asilimia 100,Kabuhoro 281 wote wameripoti Buswelu sekondari watoto 561 walioripoti asilimia 92 sawa na wanafunzi 515 huku  asilimia 8 tu ndio hawajafika.

Hata hivyo Mwalimu Mugyabuso, amesema zipo hatua zinazochukuliwa kwa mzazi endapo mtoto wake asiporipoti shuleni na kwa mzazi au mlezi anayemzuia mtoto kwenda shule anafanya kosa kisheria.

“Mwalimu Mkuu huandaa taarifa za mahudhurio, na mtoto akionekana hajahudhuria kwa siku kadhaa mzazi huitwa katika ngazi ya kata kwa hatua za kisheria,” amesema.

Ameeleza kuwa pamoja na changamoto ndogo ya miundombinu katika baadhi ya shule, hakuna mwanafunzi aliyeshindwa kuanza masomo kwa sababu hiyo, huku Serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya elimu na kuajiri walimu wapya.

Sanjari na hayo Mwalimu Mugyabuso,amesema mafanikio ya Halmashauri hiyo katika mitihani ya kitaifa yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa chakula shuleni.

“Chakula, michezo na taaluma ni vitu vinavyowahamasisha wanafunzi kuhudhuria shule. Tunashirikiana na Mkuu wa Wilaya na wazazi kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula cha mchana shuleni,”amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bujingwa,Magweiga Magabe,amesema kwa mwaka huu shule hiyo imepangiwa  wanafunzi wa kidato cha kwanza 538,kati yao wavulana 242 na wasichana 296.Hadi kufikia Februari 5,2026 wanafunzi waliopokelewa na kuingia darasani ni 360 huku wanafunzi  175  wameenda shule binafsi 175.

“Hivyo ukichukua idadi ya  wanafunzi waliopo shuleni hapa na walioenda shule binafsi inakuwa  jumla ya wanafunzi wote ambao tumepangiwa na  wameisha ripoti  shuleni ni asilimia 99.44,”amesema Mwalimu Magabe.

Amesema changamoto kubwa kwa wanafunzi wengi ni lugha ya Kiingereza, hivyo shule imeandaa mafunzo ya awali ya lugha hiyo kwa wiki sita za mwanzo.

“Tunapopokea wanafunzi hawa wametoka shule za msingi asilimia kubwa walikuwa wanatumia lugha ya kiswahili wakifika hapa tunahamia kwenye lugha ya kiingereza,kwaio kuna hali ya kubabaika katika lugha hii.

Baada ya mafunzo hayo, wanafunzi wanakuwa na uwezo wa kujifunza masomo yote kwa lugha ya Kiingereza,” amesema Mwalimu Magabe.

Pia amesema  shule hiyo  ina miundombinu ya kutosha kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo ikiwemo madarasa,viti na meza, vitabu vya kutosha na imepokea kiasi cha milioni 25 kwa ajili ya kukamilisha vyumba viwili vya madarasa.

Nao baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Bujingwa wameeleza namba walivhojipanga kukabiliana na lugha ya kiingereza katika kujifunza.

Ambapo Careen Philipo,amesema wanafunzi wengi waliotoka shule za msingi za Serikali wanakabiliwa na changamoto ya lugha ya Kiingereza, lakini amewahimiza wasikate tamaa.

“Naiomba Serikali kuona namna ya kuhakikisha inawajengea uelewa wanafunzi kufahamu lugha ya kiingereza tangu shule ya msingi ili kuondoa changamoto hiyo huku wazazi kuhakikisha wanawasimamia watoto wao na kufuatilia maendeleo yao ya shule pamoja na kutimiza wajibu kwa kuwapatia mahitaji muhimu,”amesema Careen.

Pia amewasisitiza watoto wa kike kujikita zaidi katika masomo na wajiamini kusoma masomo ya sayansi ili waweze kushindana katika soko la ajira na kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

Eunice Miguel amesema amejiandaa vyema kukabiliana na changamoto ya lugha ya  kiingereza hasa katika kipindi hiki cha mafunzo ya awali ya lugha hiyo huku akiiomba Serikali kuendelea kuongeza vitabu na vitendea kazi ili kuondoa daraja la nne na sifuri katika mitihani ya kitaifa.