November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kumuua mdogo wake

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Asteria Renatus,(34) Mkulima na mkazi wa Kitongoji cha Mwajuli, Wilaya ya Kwimba anashikiliwa na jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua mdogo wake kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali (sululu).

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Januari 21,2024 majira ya saa 6 mchana katika Hospitali ya Sumve ilioko Wilaya ya Kwimba mkoani hapa ambapo Mlingwa Renatus(15),mwanafunzi wa darasa la nne shule ya msingi Mwampulu alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu baada ya kushambuliwa na Astelia Renatus ambaye ni dada yake.

Inadaiwa kuwa wazazi ambao ni Renatus Nicholaus (64) na mkewe Julitha Ngwanchele (49) pamoja na watoto wengine walikuwa wameenda shambani kwa ajili ya kilimo na kumuacha Astelia akiwa na mdogo wake ndipo alipotenda ukatili huo.

Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa ikiwa ni pamoja na kujua utimamu wake wa akili na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Hata hivyo katika tukio jingine Mutafungwa ameeleza kuwa jeshi hilo linawashikilia watu sita kwa kosa la kughushi nyaraka mbalimbali za Serikali kwa lengo la kujipatia fedha kwa watu mbalimbali wanaotafuta nyaraka mbalimbali kwa ajili ya kupata kazi na huduma nyingine katika idara mbalimbali za Serikali.

Mutafungwa ameeleza kuwa operesheni hiyo ilianza Januari 15 hadi 19,2024 katika maeneo ya Wilaya ya Nyamagana na Ilemela ambapo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali walifanikiwa kuwakamata watu 6 wakiwa na vilelelezo mbalimbali ambavyo wamekuwa wakivitumia kughushi nyaraka hizo.

Watuhumiwa waliokamatwa ni Vedastus Faustine(54) mkazi wa Buswelu, mfanyabiashara,Joseph Ladislaus Kantanga(47) Mkazi wa Makoroboi,Lameck Pascal Bilikwija(29) Mkazi wa Kiloleli ”B”, Paul Patrick Odumbe (58) mkazi wa Igogo,Evarist Abby Leonard(28) mkazi wa Mabatini Kaskazini na Abdul Hassan Kiraka (29) mkazi wa Kawekamo Ilemela.

Watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa kwa kina na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika ambapo jeshi hilo
linawataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka pia litaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahalifu.