Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Rukwa
Jeshi la Polisi mkoani Rukwa linamshikilia mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Anifa Mwanawima (36) mkazi wa Kijiji cha Mashete wilayani Nkasi kwa tuhuma za kumtupa mtoto wake chooni baada ya kujifungua.
Huku ikielezwa kuwa tukio hilo limetokana na migogoro ya kifamilia ambapo mwanamke huyo mwenye Watoto watatu alitengana na mumewe na kwenda kupanga chumba kijijini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa Shadrack Masija ni kuwa tukio hilo limetokea jana baada ya kubainika kuwa mtoto mchanga ametupwa chooni kutokana na harufu Kali iliyokuwa ikitokea chooni ambapo Mama mwenye nyumba alitoa taarifa Kwa majirani zake pamoja na kwa viongozi wa Kijiji.
Amesema kuwa kufuatia hali hiyo baada ya kujiridhisha kuwa kilichopo ndani ya choo ni mtoto walitoa taarifa Polisi ambao walishirikiana kuiopoa mwili wa kichanga huyo kutoka ndani ya choo huku ikiwa imeharibika na kutoa harufu kali.
Kamanda Masija amesema kuwa baada ya uchunguzi wa haraka ilibainika kuwa alikuwepo mwanamke aliyekua mjamzito akiishi katika nyumba hiyo lakini walipomtizama hawakuuona tena ujauzito na kumtilia shaka na kukamatwa na katika mahojiano alikiri kuhusika katika tukio hilo la kumtupa chooni mwanae.
Amedai kuwa mwanamke huyo siku tatu zilizopita akiwa mjamzito alipata uchungu na kujifungua kwa siri bila ya mtu yeyote kujua na ndipo alipomtumbukiza chooni mtoto huyo na kufariki dunia.
Pia amefafanua kuwa kutokana na uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa mtoto huyo alikua ni wa kiume na amekaa chooni kwa muda wa siku tatu toka atupwe chooni na kuwa mwili wake uliharibika sana.
Amesema kwa sasa wanaendelea na uchunguzi zaidi na ukikamilika watamfikisha mahakamani kujibu tuhuma hizo mtuhumiwa huyo.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato