March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asenga ahoji utaratibu wa kufuata kwa wanaofanya biashara barabarani

Na Joyce Kasiki,Dodoma

MBUNGE  wa Jimbo la Kilombero,  Abubakar  Asenga, amehoji bungeni kuhusu utaratibu unaopaswa kufuatwa na wananchi wanaofanya biashara pembezoni mwa barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), hususan katika maeneo ya Mkambe, Kidatu na Mkula.

Akiuliza swqli leo Feb 5,2026 bungeni jijini Dodoma , Asenga aliuliza ni utaratibu gani rasmi unaotakiwa kufuatwa na wafanyabiashara hao ili kufanya shughuli zao kisheria bila kuvunja sheria za matumizi ya hifadhi ya barabara.

Aidha, katika swali la nyongeza, Mbunge huyo alitaka kufahamu ni lini wananchi ambao hawajalipwa fidia kupisha ujenzi wa barabara ya Ifakara–Kidatu watalipwa stahiki zao, pamoja na lini taa za barabarani katika barabara hiyo zitafungwa.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema kuwa kwa mujibu wa Marekebisho ya Kanuni za Matumizi ya Barabara za Mwaka 2025, Kanuni ya 36(4) imeweka bayana utaratibu kwa wafanyabiashara wanaotaka kutumia maeneo ya pembezoni mwa barabara.

“Mfanyabiashara yeyote anayependa kufanya biashara katika hifadhi ya barabara anatakiwa kujaza Fomu Maalum ya Maombi inayotolewa na TANROADS na kulipa ada ya maombi kabla ya kuwasilisha fomu hiyo,” amesema Kasekenya.
Ameongeza kuwa baada ya TANROADS kupokea maombi hayo, yatachakatwa na yale yatakayokidhi vigezo yatapatiwa kibali rasmi, huku mwombaji akiarifiwa gharama atakazotakiwa kulipa kwa mujibu wa sheria husika.

Kuhusu suala la fidia, Naibu Waziri huyo amesema kuwa Serikali imeunda kamati maalum chini ya uongozi wa Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya wananchi ambao hawajalipwa au waliopunjwa fidia wakati wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Ifakara–Kidatu.

Amesema kuwa baada ya malalamiko kuwasilishwa na Serikali kujiridhisha kuwa walalamikaji wanastahili kulipwa, malipo yao yatafanyika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Katika suala la uwekaji wa taa za barabarani, Kasekenya amebainisha kuwa Serikali ina utaratibu wa kuhakikisha barabara zote mpya, hususan zile zinazopita maeneo ya mijini, zinawekewa taa za barabarani.

“Barabara ya Ifakara–Kidatu ni miongoni mwa barabara hizo, hivyo itawekewa taa za barabarani kwa mujibu wa mpango wa Serikali,” amesema.