March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asas ashtushwa kusuasua mradi soko la Matola

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Salim Asas, ameeleza kusikitishwa na kusuasua kwa ujenzi wa Soko la Matola licha ya mradi huo kuwa na fedha zote za utekelezaji, na ameahidi kuwasilisha taarifa ya hali halisi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza Februari 4, 2026 wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali jijini Mbeya katika kuadhimisha Miaka 49 ya CCM, Asas alisema haiwezekani mradi mkubwa na muhimu kama huo kuendelea kutokamilika wakati fedha zimetolewa kikamilifu.

“Katika mwongozo tulioupata kwenye kikao cha Kamati Kuu Taifa, tulielekezwa kukagua miradi yote katika maadhimisho ya Miaka 49 ya CCM. Mwenyekiti wetu wa Taifa, Rais Dkt. Samia, amesisitiza kuwa fedha nyingi zimepelekwa mikoani lakini baadhi ya miradi imeshindwa kukamilika kwa wakati,” amesema Asas.

Amesema kuwa Rais Samia amewataka viongozi wote wa Kamati Kuu kufuatilia miradi isiyokamilika na kutoa taarifa zake moja kwa moja.

“Sasa nikiwa hapa Mbeya, nitasema kile nilichokiona. Mkandarasi hafanyi kazi kulingana na masharti ya mkataba. Nitaandika taarifa ya kina na kupeleka kwa Rais kuwa mradi wa Soko la Matola unasuasua, na chama kinafuatilia kwa karibu,” amesema.

Changamoto za Usimamizi wa Fedha

Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dour Mohamed, alisema mkandarasi wa mradi huo — Kampuni ya Siho Tech Engineering Co. Ltd — ameshindwa kusimamia fedha za mradi ipasavyo.

Amesema si kweli kwamba mradi unaweza kukamilika Mei mwaka huu kutokana na ucheleweshaji uliojitokeza, ikiwemo madai ya kuhamishwa kwa baadhi ya fedha za mradi kwenda kwenye shughuli nyingine.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Ndele Mwaselela, amepinga madai ya kukamilika kwa wakati huo huo akisema kasi ya ujenzi ni ndogo kutokana na idadi finyu ya wafanyakazi eneo la mradi.

“Huwezi kutegemea kukamilika kwa mradi mkubwa kama huu kwa kasi hii. Wafanyakazi ni wachache sana na maendeleo hayaendani na muda uliobaki,” alisema Mwaselela.

Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Annamary Joseph, amesema  mradi huo ulipaswa kukamilika Agosti 31, 2025, lakini mapitio ya michoro na kuongezeka kwa kazi ya sakafu ya juu ambayo haikuwepo kwenye mchoro wa awali yamesababisha ucheleweshaji.

Amesema pia kuwa mvua zinazoendelea kunyesha zimepunguza kasi ya ujenzi.

Hata hivyo, alisema mkandarasi ameongezewa muda hadi Mei 28, 2026, na sasa amelazimika kufanya kazi usiku na mchana huku akitakiwa kuongeza idadi ya wafanyakazi ili kuongeza kasi.

Mradi wa Soko la Matola ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati jijini Mbeya na unatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi mara tu utakapokamilika.