January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Arusha wamshurukuru Rais Samia kwa majiko ya gesi

Na Penina Malundo,Timesmajiraonline

WANANCHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha wamemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi wa kusambaza majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50 katika halmashauri hiyo.

Wametoa pongezi hizo jana mkoani humo,wakati wa utekelezaji wa mradi wa kusambaza majiko ya gesi yanayotolewa kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50 na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ushirikiano na Kampuni ya Lake Gas wilayani humo.

Walisema mradi umefika wakati mzuri kwani kwa sasa upatikanaji wa mkaa ni mgumu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kwamba inasababisha kupanda kwa gharama za maisha.

“Tumefurahi kufikiwa na mradi, suala la kuni na mkaa hapa kwa sasa ni shida; tunatumia muda mrefu kuwasha moto maana kuni ni mbichi,” alisema Neema Rumas Mkazi wa Kijiji cha Siwandeti.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Siwandeti, Daniel Mitiwek,i alisema ujio wa mradi huo ni mkombozi wa mazingira kwani suala la ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa limekithiri katika kijiji hicho lakini kufuatia mradi huo miti inakwenda kusalimika.

Akizungumza wakati wa zoezi la usambazaji na uuzwaji wa majiko hayo ya ruzuku wilayani humo, Msimamizi wa Mradi wa REA Kanda ya Kaskazini (Kilimanjaro na Arusha), Mhandisi Gift Kombe aliwasisitiza wananchi kuzingatia elimu inayotolewa ya matumizi sahihi ya majiko hayo ili yaweze kuleta tija inayokusudiwa ikiwa na kuendelea kujaza mitungi hiyo pindi inapoisha.

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ambao ulizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi Mei mwaka huu.