Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
APPS and Girls kwa kushirikiana na Yas Tanzania wameadhimisha mahafali ya kundi lingine la wahitimu wa programu ya Jovia, mpango unaolenga kuwawezesha wasichana kupitia teknolojia na ujasiriamali.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019, Jovia imekuwa jukwaa muhimu kwa wasichana kupata ujuzi wa kidigitali, maarifa ya biashara, na ushauri, hatua inayochangia kupunguza pengo la kijinsia katika nyanja za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, na Hisabati (STEM).
Mwaka huu, programu ya Jovia imefanikiwa kuwahusisha wasichana 35 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania, wakiwemo 18 kutoka nje ya Dar es Salaam.

Ili kuhakikisha mazingira salama ya kujifunzia, Apps and Girls ilianzisha hosteli ya malazi kwa washiriki wanaotoka mbali, jambo lililowezesha ushiriki wao katika mafunzo kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, mgeni rasmi amepongeza jitihada za Apps and Girls na Yas Tanzania kwa kuwezesha vijana wa kike kufikia ndoto zao.
“Jovia inabadilisha maisha! Mafanikio ya wahitimu wetu yanaonesha kuwa wakati wasichana wanapowezeshwa, wanageuza ndoto kuwa uhalisia na kuchangia maendeleo ya jamii zao,” amesema na kuongeza
“Wahitimu 7 wamepata ajira na wanajiunga na soko la ajira wakiwa na ujuzi wa kutosha. Wahitimu 5 wanaendelea na elimu ya juu, wakichukua hatua zaidi za maendeleo binafsi.

“Wahitimu 25 wameanzisha biashara zao, wakitumia maarifa waliyojifunza kubuni na kukuza miradi yao,”.
Kwa upande wake, Apps and Girls imetoa shukrani za dhati kwa Yas Tanzania kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha programu hii.
“Tunashukuru kwa msaada wa wadau wetu ambao wamekuwa sehemu ya mafanikio haya. Ushirikiano huu unatoa fursa kwa wasichana wengi zaidi kuingia kwenye sekta ya teknolojia na ujasiriamali,” imesema Apps and Girls.
Wahitimu wa Jovia 2025 wamehimizwa kuendelea kutumia ujuzi walioupata kwa manufaa yao binafsi na jamii kwa ujumla.
“Hii ni hatua moja tu katika safari yenu. Tunawaamini kama viongozi wa kesho, wavumbuzi, na wabunifu wa suluhisho zitakazobadilisha dunia.”


More Stories
Matokeo ya usaili TRA kutangazwa April 25
Waziri Mavunde azindua rasmi shughuli za uchimbaji madini Porcupine North -Chunya Mbeya
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Baraza la Taifa la Ujenzi waingia makubaliano ya mashirikiano sekta ya ujenzi