Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Itilima
“POPOTE nitakapokutana na Rais Samia Suluhu Hassan, nitamshukuru sana kwa kazi kubwa anayoifanya, kwenye familia yangu hatuwezi kuisahau TASAF.”
Hiyo ni kauli ya mnufaika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Regina Malisa (52), ambaye sasa anaomba aondolewe kwenye mpango huo baada kuanzisha mradi unaomwezesha awe na uhakika wa kujiingizia kipato.
Bi. Regina mkazi wa Kijiji Itumbilo, Kata ya Ruguru Halmashauri ya Wilaya Itilima katika Mkoa wa Simuyu, amefikia uamuzi huo ili kutoa nafasi kwa watu wengine wenye hali ngumu kiuchumi kama aliyokuwa nayo yeye, waweze kufaidika kupitia mpango huo.
Bi. Regina ambaye ni mama wa watoto nane alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizungumza na waandishi wa habari akieleza jinsi TASAF ilivyomuondoa kwenye umaskini.
“Kwa hatua ambayo nimefikia namshukuru Mwenyezi Mungu, naomba kujiuzulu TASAF, nalishukuru sana shirika hili (TASAF), namuomba Rais Samia shirika hili, liendelee kuwepo, linawasaidia Watanzania wengine.”
Akieleza hali aliyokuwa nayo awali na sasa hadi anafikia kuomba aondolewe kwenye mpango huo, Regina alisema alikuwa na maisha magumu, alikuwa anafanya vibarua kwenye miji ya watu, ndipo watoto wake waweze kupata mahitaji ya shule.
Mbali na kufanya vibarua, Regina alisema alikuwa anauza gongo, biashara ambayo alikuwa anakatazwa na mama yake, lakini kwa sababu ya maisha magumu alilazimika kuifanya.
“Nilifanya hivyo kwa sababu mume wangu hana ajira, anasubiri mwezi wa saba aende kwenye kilimo cha pamba, nikaona nijiingize kwenye kuuza gongo,” anasema Regina.
Kuhusu vibarua, anasema alikuwa anasubiri hadi wenzake walime kwanza awafanyie vibarua ili apate hela ya kuhudumia familia yake na fedha za kununulia mbegu, ndipo aanze kilimo.
Kwa upande wa mazingira ya kulala, Bi. Regina alisema yalikuwa shida, kwani walikuwa wanalala chumba kimoja yeye, mume wake na watoto nane.
“Lakini mwaka 2015 ilipokuja TASAF, Mwenyezi Mungu akanibariki, nilipopata ruzuku kutoka TASAF ndipo alipata nguvu ya kuanzisha mradi wa kutengeneza sabuni za maji na kuuzia wananchi,” alisema na kuongeza kuwa kuanzia hapo watoto wake walianza kusoma vizuri tu.
Alizidi kufafanua kwamba aliendelea hivyo hivyo, ambapo alianza kulima pamba. Wakati anaendelea na kilimo, alisema kwenye kijiji chao walipelekewa mradi wa kuchimba visima, ambapo walengwa wa TASAF walikuwa wakifanyakazi kupitia ajira za muda.
Bi. Regina anasema hela aliyokuwa akilipwa ilimpa nguvu, kwani alipolipwa fedha hizo alinunua vitambaa kwa ajili ya kutengeza batiki na madawa yake.
“Baada ya kuanzisha mradi wa kutengeneza batiki, mtaji wangu ukawa mkubwa, faida nikaipeleka kwenye kilimo cha karanga na nilipovuna na kuuza, nikanunua cherehani na kuanza ushonaji kwenye nyumba za watu kwa muda wa miaka miwili.
Wakati huo nilikuwa sijapata wazo la kufungua ofisi, biashara zake zilikuwa za kutembeza.”
Baadaye anasema alilima shamba ekari mbili akalima pamba na alipovuna na kuuza alipata sh. 1,000,000. Alipopata hela hiyo na faida nyingine aliyokuwa akipata kutoka kwenye biashara zake, akaamua apange flemu.
Anasema hela zilizobaki alinunua nguo, viatu, mikoba na vitu vingine akawa amefungua duka. “Hata zile fedha ambazo nilipewa na TASAF nilikuwa naziingiza kwenye duka,”anasema.
Anasema biashara yake hiyo ya duka na ushonaji imemwezesha kusomesha watoto wake, ambapo mmoja yupo kidato cha sita, mwingine yupo kidato cha kwanza mkoani Dodoma ambako anasoma shule ya vipaji maalum.
Anasema watoto wengine wanne wanasoma shule ya msingi Itubilo.” Kwa kweli TASAF imenisaidia, kwani kama mwanafunzi anahitaji kitu chochote, anakipata tofauti na zamani.
Anasema alianza kupata ruzuku ya TASAF akilipwa sh. 52,000 ikaongezeka hadi sh. 62,000 ikapanda tena ikawa sh. 76,000.
“Nilipofika kwenye sh.76,000 na huku pembeni nina hela ya miradi mambo yakawa mazuri,” anasema. na kuongeza; “Mfano ukiwa na mtaji wa sh. 150,000 ukaupeleka kwenye biashara baadaye utakuwa na sh. 200,000, kwa hiyo utakuwa umepata mahitaji ya familia yako na mtaji kubaki umesimama,”anasema Bi. Regina.
Anatoa ushauri kwa wanufaika wa TASAF kutambua kuwa hela wanayolipwa, sio ndogo, ni kubwa, kama mtu hana akili ya kuzizungusha hizo hela, hata akipewe milioni ataona ni hela ndogo.
“Lakini hata ukiwa na 50,000 ukienda kununua miwa ya kuuza ukishaanza kuiuza utapata na faida, hivyo haitakuwa sh. 50,000 tena,”anasema na kuongeza;
“Wakati unazungusha hizo sh. 50,000 utakutana na hela ya TASAF imefika, unaongezea mtaji. Unachotakiwa ni kujitaidi.”
More Stories
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu
RC Mrindoko:Ufyekaji wa mahindi Tanganyika si maelekezo ya serikali
Walimu S/ Sekondari Ilala wafundwa juu ya maadili ya wanafunzi