December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mabula kuboresha afya jimbo la Ilemela (+video)

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

MIKUTANO ya kampeni ya kuomba kura inaendelea huku mgombea ubunge Jimbo la Ilemela kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Angeline Mabula amesema kuwa amefanikiwa kuboresha sekta ya afya na ataendelea kuboresha katika jimbo hilo endapo atapatiwa ridhaa kwa awamu ya pili.

Akizungumza katika mikutano yake ya kampeni (bofya kuangalia video hapo juu) wa kuomba kura kwa wananchi,uliyofanyika Nyamlekerwa Kata ya Mecco na Kiseke A kata ya Kiseke, amesema wakati wanaingia madarakani mwaka 2015 Jimbo hilo lilikuwa na vituo vya afya viwili ambavyo havijaboreshwa.

Amesema,lakini leo hii vituo hivyo vya afya vya Karume na Buzuruga vimeboreshwa kwa kiasi kikubwa, ambapo cha Buzuruga kimewekwa chumba cha upasuaji ambapo mama wajawazito wakienda pale wakishindwa kujifungua kawaida watafanyiwa upasuaji hapo hapo hakuna haja ya kupelekwa Sekou-Toure au Bugando.

“Utajifungulua pale pale, theatre ipo, maabara ipo,wodi zipo,jengo la mama na mtoto lipo, nyumba za wafanyakazi zimetengewa hapo kwaio hakuna shida tena,sasa hivi kimetengewa milioni 70 kwa ajili ya kuendelea kukiboresha na kuweka uzio kwenye kituo chenu cha afya Buzuruga, amesema Dkt.Angeline.

Pia amesema,katika Kata ya Buswelu palipokuwa pametengwa eneo la kujengea hospitali ya wilaya ambapo jengo la wagonjwa wa nje lilikuwa limekamilika kinaenda kuwa kituo cha afya hivyo kuongeza idadi ya vituo vya afya jimboni humo na kusaidia kupunguza msongamano katika hospitali ya wilaya.

Hata hivyo amesema,hospitali ya Wilaya ya Ilemela imejengwa Isandu ambapo zaidi ya sh. bilioni 2.8 zimetumika ambapo sh.bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa majengo 7 ambayo yamekamilika, sh.bilioni 1 zimetengewa kwa ajili ya vifaa tiba ikiwemo X-RAY mashine na Utral- sound mashine huku milioni 46 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ambapo itasaidia ata kama mvua inanyesha mtu asinyeshewe kwa vile majengo yapo mbalimbali.

Kwa upande wake Meneja Kampeni wa CCM Jimbo la Ilemela Kazungu Idebe amesema miradi iliyotekelezwa kwa kipindi cha miaka tano ya Dkt.John Magufuli akisaidiana na Dkt.Angeline katika jimbo hilo katika sekta ya afya ni ujenzi wa hospitali ya wilaya,zahanati mpya tano na uboreshwaji wa vituo vya afya Karume na Buzuruga,hivyo amewaomba wananchi kuchagua wagombea wa CCM ili waweze kushiriki na kwa pamoja kusukuma maendeleo kwani sasa wamefungwa injini ya trekta.

Meneja Kampeni wa CCM Jimbo la Ilemela Kazungu Idebe katikati akimnadi kwa wananchi wa kata ya Kahama mgombea Ubunge Jimbo la Ilemela kupitia CCM Dkt.Angeline Mabula(kushoto) na Diwani wa Kata ya Kiseke Mwevi Ramadhani (kulia) kwenye mkutano wa kampeni wa kuomba kura kwa wananchi uliofanyika Kata ya Kiseke. Picha na Judith Ferdinand