Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora
KAMPUNI ya ununuzi wa zao la tumbaku ya Alliance One Tobacco Tanzania Ltd (AOTTL) imeunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kuokoa mazingira kwa kupanda miti zaidi ya milioni 1 kwenye eneo lenye ukubwa wa hekta 425, Wilayani Nzega Mkoani hapa.
Akitoa taarifa za mafanikio hayo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu Godfrey Mnzava juzi, Afisa Misitu wa Kampuni hiyo Rashid Salumu alisema kuwa wamepanda miti hiyo katika msimu wa mwaka 2023/2024.
Amesema kuwa mradi huo uliogharimu zaidi ya sh mil 980 umekuwa kichocheo kikubwa cha utunzaji mazingira katika Wilaya hiyo na maeneo mengine kwani wakulima wote wanaolima zao hilo wamepewa miche ya kupanda katika maeneo yao.
Ameeleza kuwa Kampuni hiyo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya Nzega wamebeba agenda ya kuhimiza mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira hususani misitu na kuhakikisha sekta binafsi zinashiriki kikamilifu katika kulinda na kuhifadhi misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Salumu amebainisha kuwa mradi huo kwa mara ya kwanza ulianza kutekelezwa Wilayani humo mwaka 2022 katika Kata ya Nkiniziwa ambapo walianza kwa kusafisha eneo, kuchimba mashimo na kupanda miti aina ya Mfudufudu.
Katika msimu huo wa 2022/2023 jumla ya miti 110,923 ilipandwa kwenye eneo lenye ukubwa wa hekta 44.3 na takribani miti 91,923 sawa na asilimia 83 ilikua ila miti 18,287 sawa na asilimia 17 ilikufa kutokana na mvua kubwa na miti kuoza.
‘Tunamshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhimiza mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira hususani misitu na kutoa fursa kwa Kampuni binafsi kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa misitu’, amesema.
Akiongea baada ya kukagua na kushiriki zoezi la upandaji miti katika eneo hilo la mradi lililopo katika kata ya Nkiniziwa, Nzega, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mnzava amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Kampuni hiyo.
Aidha amesisitiza kuwa suala la utunzaji mazingira ni la kila mtu, hivyo akaitaka jamii kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa kushiriki kikamilifu kupanda miti katika maeneo yao.
Amebainisha kauli mbiu ya Mbio hizo mwaka huu kuwa ni ‘Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa endelevu, hivyo akisisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini Novemba 25 mwaka huu hapa nchini.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto