Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mwanza
Mkazi wa Nyasaka wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Philipo Mhina (52), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza na kusomewa shtaka la kuendesha gari kwa uzembe katika barabara ya Umma na kusababisha kifo cha askari wa Usalama Barabarani, WP 3984. Sajenti, Stella Alfonce.
Philipo amesomewa shtaka hilo leo Novemba 10, 2023 katika kesi ya jinai namba 36752/2023 ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 41, 63 (2) (b) na 27 (1) (a) cha Sheria ya Usalama Barabarani sura 168 marejeo ya mwaka 2002.
Mbele ya hakimu mkazi Mwandamizi Amani Sumari, mwendesha mashtaka wa serikali Monika Mweli amesema mshtakiwa alitenda kosa hilo Novemba Mosi, 2023 eneo la Nyamhongoro wilaya ya Ilemela.
Mhina ambaye ni dereva wa gari ya Shule ya Msingi Nyamuge ya jijini Mwanza akiwa anarudisha nyuma gari hiyo yenye namba za usajili T.964 BRJ aina ya Mitsubishi Rosa baada ya kukamatwa na kosa la usalama barabarani alimgonga Sajenti Stella na kusababisha kifo chake.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa amekana na kurejeshewa rumande kutokana na kutokidhi vigezo vya dhamana ambapo alitakiwa kuwa na wadhamini wawili na barua ya mwenyekiti wa serikali ya mtaa kila mmoja.
Hakimu Sumari, ameahirisha shauri hilo hadi tarehe 23.11.2023 litakapokuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya shtaka linalomkabili.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM