Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
MAHAKAMA ya Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya imemhukumu kifungo cha maisha Change Mawanga(32) mkazi wa Mlimanjiwa Kata ya Mbugani kwa kosa la kumbaka na kumlawiti mtoto wa dada yake mwenye umri wa miaka minne na kumsababishia maambukizi ya magonjwa ya zinaa.
Akisoma makosa ya mtuhumiwa katika kesi ya jinai namba 64/2022 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya James Mhanuzi,Mwendesha mashitaka wa Polisi Mazoya Luchagula ameiambia mahakama kuwa mshitakiwa ametenda makosa hayo kwa nyakati tofauti mwezi aprili 2022 ambapo alikamatwa mei 5,2022.Mazoya amesema makosa hayo ni kinyume cha sheria namba 130(1)(2) na 131(1)sura ya 16 ya makosa ya jinai iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019 ambapo mshitakiwa alikana makosa yote.
Upande wa mashitaka umeleta mashahidi mbalimbali akiwemo mtoto aliyefanyiwa ukatili huo ambapo alimtamtambua mahakamani kama anko,mama wa mtoto,askari,afisa ustawi wa jamii na daktari aliyewasilisha PF 3 iliyoambatana na vipimo vilivyoonesha mtoto kubakwa na kuingiliwa kinyume cha maumbile.
Baada ya Hakimu James Mhanuzi kusikiliza upande wa mashitaka na mshitakiwa mahakama iliridhika pasipo shaka na upande wa mashitaka pia kubaini kuwa mshitakiwa anayo kesi ya kujibu.
Akijitetea Change Mawanga amesema kuwa hakutenda makosa hayo na kwamba anasingiziwa tu na katika maombolezo yake aliiomba mahakama kumwachia huru kwa kuwa ana wategemezi akiwemo mama yake,mke na wadogo zake wanaomtegemea.
Kwa upande wa mashitaka Mazoya Luchagula amesema mbali ya mshitakiwa kutokuwa na matukio mengine ya uhalifu ameiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa hasa ikizingatiwa mtoto aliyefanyiwa ukatili ana umri wa miaka minne tu isitoshe ni mtoto wa dada yake.
Aidha Hakimu James Mhanuzi baada ya kusikiliza pande zote mahakama imemtia hatiani kwa makosa yote mawili ambapo kosa la kumbaka mtoto chini ya miaka 18 kifungu cha sheria 154(1)(2) sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022 adhabu yake ni kifungo cha maisha.
Kosa la pili la kumlawiti mtoto chini ya miaka 18 adhabu yake ni kifungo cha maisha.
Mhanuzi amesema adhabu hiyo iwe fundisho kwa mshitakiwa na wengine wanaojihusisha na vitendo hivyo hasa kutokana na kukuthiri vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto Wilayani Chunya vitendo vinavyohusishwa na imani za kishirikina kwa madai ya kupata dhahabu pindi wanapojamiana au kuwalawiti watoto wadogo.
Hivyo kwa makosa yote mshitakiwa atatumikia adhabu zote mbili kwa pamoja na maisha yake yote kuishia gerezani.
Nje ya mahakama Afisa Ustawi wa Jamii Nashitabo Mwalende amesema mahakama imetenda haki kwani kumekuwa na vitendo vingi vya ukatili dhidi ya watoto.
Mahakama hiyo bado inaendelea kusikiliza kesi za ubakaji na ulawiti ikiwemo ya baba kumbaka mwanawe hukumu itakayotolewa mwezi agosti mwaka huu.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best