December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Simiyu mbaroni tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wa chuo

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza 

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Yahaya Esmail Nawanda (46) mkazi wa mtaa wa Nyaumata – Bariadi mkoani humo ameshikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa tuhuma za kumuingilia kimwili kinyume na maumbile mwanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine(SAUT),mkoani hapa.

Ambapo tukio hilo lilitokea mnamo Juni 02,2024 majira ya usiku eneo la Rock City Mall, mtaa wa Ghana, wilayani ya Ilemela mkoani hapa

Akizungumza na waandishi wa habari leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza  DCP Wilbroad Mutafungwa,amesema   jeshi hilo limefanikiwa kumkamata  Nawanda Juni  13,mwaka huu, majira ya saa 6:00 mchana jijini Mwanza,akidaiwa kutenda kosa hilo ambapo anahojiwa na taasisi za kiuchunguzi ukiwemo wa kisayansi.

“Tunamshikilia Yahaya Ismail Nawanda kwa mahojiano na upelelezi unaokwenda sambamba na uchunguzi wa kisayansi,ukikamilika jalada litapelekwa ofisi ya Mashitaka kwa hatua zaidi za kisheria,”amesema Mutafungwa.

Hata hivyo Mutafungwa ameeleza kuwa kuhusu waraka unaosambaa mitandaoni kuwa mtendewa wa ukatili huo ameamua kuondoa shauri hilo kwa hiari yake bila shinikizo la mtu yeyote na hataki kutumika kisiasa,amesema taarifa hiyo si sehemu ya uchunguzi wala ushahidi wao.

“Jeshi la polisi tumeona hako ka taarifa, matukio ya ukatili mlalamikaji ni Jamhuri na mtendewa ni shahidi,taarifa hiyo ni ya mitandaoni  haikupokelewa polisi na si sehemu ya upelelezi wa jalada letu,hivyo mashauri hayo ya ukatili mlalamikaji ni Jamhuri mtendewa anabaki kuwa shahidi,”amesema.

Kamanda huyo wa polisi amesema yanafanyika mawasiliano ya kulileta gari linalodaiwa kutumika kufanyika ukatili huo kwa sababu ni sehemu ya vielelezo vya upelelezi na wakati ukifika vitaoneshwa kama sheria inavyoelekeza.

“Uchunguzi unaendelea na tutachunguza pia umiliki wa gari hilo, vyombo vya uchunguzi vikikamilisha vitatupa taarifa kwa maandishi,”amesema.

Mutafungwa ameeleza kuwa kuhusu taarifa kuwa Wakili mmoja anayedaiwa kuingilia kati kufanya negotiation (majadiliano) na mtendewa wa tukio hilo kwamba ndio chanzo na sababu ya mwanafunzi huyo kuandika waraka huo akiomba kuondoa kesi hiyo polisi,amesema katika ushughulikiaji wa matukio ya ukatili hakuna majadiliano,msingi wake ni Jamhuri pekee.

“Makosa haya ni tofauti na matusi (mtu kutukana au kutukanwa),anaweza kufanya negotiation na si makosa yanayohusu ukatili wa kijinsia na watoto, hivyo hilo halijawahi kufanyika katika mazingira ya jeshi la polisi na halina uhusiano na upelelezi wa kesi yetu,”amesema na kuongeza;

“Upelelezi umekaaa vizuri na umefanyika kwa weledi wa hali ya juu katika mnyororo wa haki jinai.Subirini ukamilike mtaona kitakachofanyika,lakini kwa ushahidi wa hilo (la makubaliano) hatutaki kesi yetu iharibike,”.

Aidha wakati polisi ikitihibitisha kumkamata Nawanda,tayari Mamlaka ya uteuzi imeshatengua uteuzi wake ingawa taarifa hiyo iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano-Ikulu,haikueleza sababu ikiwa ni siku moja tangu kusambaa kwa taarifa mitandaoni akituhumiwa kumlawiti mwanachuo huyo wa SAUT.

Mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza anayesomea Shahada ya Ugavi na Manunuzi baada ya tukio hilo  alifungua jalada polisi lenye namba MZR/CID//PE/74/2024,kitendo anachodai kufanyiwa katika maegesho ya magari ya baa ya The Cask eneo la Rocky City Mall ambapo inadaiwa alifanyiwa ukatili ndani ya gari lenye namba T496 BND, aina ya Toyota Crown majira ya usiku.