January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aliyekuwa kamishna dawa za kulevya aapishwa kuwa DC Tanga

Na Hadija bagasha, Timesmajira Online

Aliyekuwa Kamishna wa Dawa za Kulevya Nchini, James Wilbert Kaji ameapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga katika hafla iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba na kuhudhuriwa na Viongozi Mbalimbali wa Serikali, Halmashauri, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wakuu wa Idara pamoja na Viongozi wa Dini

Julai 2, 2023 Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan alimteua James Wilbert Kaji kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga akichukua nafasi ya Hashim Mgandilwa ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilindi.

Katika hafla hiyo ya uapisho Mkuu wa Mkoa Tanga Waziri Kindamba amewataka viongozi Mkoani Tanga wasitumie vibaya madaraka na mamlaka waliyonayo kuwasweka rumande wananchi kwa uonevu na badala yake watumie hekma na busara katika uongozi wao.

“Nimeshalisema hili mara kadhaa sitarajii katika wakati wangu nikiwa kama Mkuu wa Mkoa kusikia watu wanawekwa wekwa ndani wanawekwa kwenye vituo vya polisi bila ya kuwa na makosa ya maana na kadri Mwenyezi Mungu anapokujaalia madaraka zaidi yapaswa sana kumuomba hekma na busara maana madaraka bila hekma na busara unaweza kuwaumiza watu wengi sanaa lakini utakaowaumiza wapo watakaonung’unika sasa katika hao watakaolalamika huwezi kutoka salama maana wapo watu dua zao na sala zao wakiomba zinakwenda kama zilivyo hakuna pazia Mungu anazipokea moja kwa moja, “alisisitiza RC Kindamba

Kwa upande wake Mwenyekiti wa ccm Mkoa Tanga Rajab Abrahaman Abdallah amewaasa viongozi Mkoani humo kudumisha amani iliyopo na kuwachukulia hatua wale wote wanaoonekana kuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani.