
Na Moses Ng’wat, Tunduma
MKAZI wa Kata ya Katete, mjini Tunduma, Songwe, Nehemia Mwazembe, anayedaiwa kujifanya mtumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), amenaswa akiwa juu ya nguzo za umeme akiendelea kuwaunganishia wateja huduma hiyo.
Mwazembe anadaiwa kukusanya Sh milioni moja kutoka kwa wateja aliokuwa akiwaunganishia umeme katika Mtaa wa Nakaumba, mjini Tunduma, baada ya kuwashawishi kwa ahadi ya kuwaunganishia huduma hiyo.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kukamatwa na maofisa wa usalama wa TANESCO Septemba Mosi, 2026, akiwa juu ya nguzo akifanya kazi ya kuwaunganishia wananchi umeme.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Kitengo cha Usalama TANESCO Mkoa wa Songwe, Juma Mauba, amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya kuwepo malalamiko ya muda mrefu ya wateja kutapeliwa fedha kwa ahadi ya kuunganishiwa umeme.
Aidha, amewataka wananchi kuthibitisha utambulisho wa mtu anayejitambulisha kuwa mtumishi wa TANESCO kabla ya kumpatia fedha kwa ajili ya huduma ya umeme.

Mauba amesema taratibu za kumfikisha mtuhumiwa huyo kwenye vyombo vya sheria zinaendelea, huku akiwataka wananchi kuwa waangalifu wanapohitaji huduma za umeme.
Katika utetezi wake, Mwazembe amesema ugumu wa maisha ndio uliomsukuma kujiingiza katika vitendo hivyo.

More Stories
Tanzania,Uganda zapiga hatua kiwanda cha kusafisha mafuta
Kamati ya Bunge:Hatutakaa kimya miradi ya Umwagiliaji
CEOs Forum yawa jukwaa la kuchochea Dira 2050