Na Allan Ntana, TimesMajira Online, Tabora
JESHI la Polisi Mkoani Tabora limemkamata Ramadhan Juma (65) mkulima, mkazi wa kijiji cha Ndekela kata ya Tongi tarafa ya Puge wilayani Nzega Mkoani humo kwa tuhuma za kukodisha silaha aina ya SMG kwa majambazi.
Hayo yamebainishwa jana na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, ACP Barnabas Mwakalukwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali.
Amesema kuwa silaha hiyo namba TZCAR 36462 na risasi zake 4 ilikamatwa Juni 19 mwaka huu saa 11.30 za jioni ikiwa imehifadhiwa katika nyumba ya mtuhumiwa huyo ambapo alikuwa akiikodisha kwa wahalifu waliokuwa wakiitumia katika matukio ya wizi na unyang’anyi.
Amebainisha kuwa baada ya kufanya msako wa kina walifanikiwa pia kumkamata Athuman Salum (30) mnyamwezi, mkulima mkazi wa kijiji cha Ndekeli na wenzake tatu ambao wamekuwa wakijihusisha na matukio ya ujambazi kijijini hapo.
Kamanda Mwakalukwa alifafanua kuwa baada ya kupekuliwa katika makazi yao watuhumiwa hao walikutwa na vipande vya nondo, visu 4 na mapanga ambavyo hutumika kutekeleza kazi zao za kihalifu.
Aidha ameongeza kuwa katika msako huo zilipatikana fedha taslimu sh. 500,000 zikiwa zimefichwa uvunguni mwa kitanda cha mtuhumiwa huyo, ambapo zinasadikika kuwa ziliporwa kwa wananchi katika tukio la ujambazi lililofanyika hivi karibuni kijijini hapo.
Ameeleza kuwa upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea na watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa na Jeshi la Polisi na punde upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
Amebainisha kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na ushirikiano mzuri wa wananchi kwa jeshi hilo, hivyo akatoa wito kwa jamii kuendelea kutoa ushirikiano zaidi ili kukomeshwa kwa matukio ya uhalifu katika wilaya zote za mkoa huo huku akiwahakikishia kuwa watoa taarifa wataendelea kulindwa.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa