Na Martha Fatael, Timesmajira Online,Moshi
WAZIRI wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, amewahakikishia usalama wa ajira zao watumimishi zaidi ya 276 waliokua wanafanyakazi chini ya kampuni ya KADCO iliyokua ikiendesha shughuli zake katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa zaidi ya miaka 25.
Kauli hiyo ya Prof. Mbarawa imekuja baada ya uwanja huo wa KIA kurudishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini (TAA)ambapo serikali kupitia Bunge iliitaka serikali isimamie kiwanja hicho cha ndege ili kuongeza ufanisi na tija katika sekta ya uchukuzi na utalii.
Akizungumza na watumishi hao Prof.Mbarawa amesema mabadiliko yaliyofanyika hayata athiri ajira ya mtumishi yeyote kwani serikali inatambua jitihada zao katika kukuza maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Amesema serikali imefanya hivyo kwa nia njema lengo likiwa ni kuboresha utoaji wa huduma bora zaidi hususani ya miundombinu ya uwanja huo ikiwemo taa, uzio pamoja na kujenga jengo la kusubiria (terminal three) la kisasa ili kukuza utalii wa ndani na nje ya nchi.
“Serikali itahakikisha yale yote mazuri yaliyokua yakifanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi yataendelea pamoja na kutilia mkazo maeneo ambayo yameonekana kusuasua hasa kwenye vitengo mbalimbali.” Amesema Mbarawa
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mussa Mbura, amesema wamepokea jukumu hilo la kusimamia, kuendesha na kuendeleza viwanja vya ndege nchini na kwamba KIA inakua miongoni mwa viwanja 59 wanavyovisimamia.
Mbura ameongeza kuwa mabadiliko yaliyofanyika juu ya uhamisho wa wafanyakazi na watumishi kutoka kampuni iliyokua inawasimamia ya KADCO kwenda TAA ni mchakato ambao serikali inaufanya kila yanapotokea mabadiliko kama hayo kwa mujibu wa taratibu na sheria za utumishi wa umma.
Juma Kimwaga ni kiongozi wa wafanyakazi KIA ameishukuru serikali kwa kuwahakikishia usalama wa ajira zao kupitia ujio wa Waziri Mbarawa kumewapa ari zaidi ya kiutendaji na wako tayari kufanyakazi mahali popote kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
“Tunaomba serikali iendeleee kutambua zaidi umuhimu wetu wafanyakazi wa KIA katika kuongeza ufanisi eneo la kiutendaji na miundombinu kupitia mabadiliko haya kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo,”amesema Arbogast Mafarasa.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua