November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo. Kulia ni Simon Jumbe (43) mkazi wa eneo la Kisasa Jijini Dodoma

Ajifanya Ofisa wa TAKUKURU, atiwa mbaroni

Na Mwandishi Wetu

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma inamshikilia, Simon Jumbe (43) mkazi wa eneo la Kisasa, Jijini Dodoma kwa tuhuma za kujifanya Ofisa wa TAKUKURU kinyume na Kifungu cha 36 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya mwaka 2018.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo, ilieleza kwamba mara kadhaa
tumewataka wakazi wa Dodoma kuwakataa na kutoa taarifa za matapeli au watu wanaojiita maofisa wa TAKUKURU ambao wamekuwa wakiichafua Taasisi hiyo kwa vitendo vyao ambavyo ni kinyume na maadili ya utendaji wa TAKUKURU.

“Katikati ya Aprili mwaka huu, tulipokea taarifa kwamba mtuhumiwa
Jumbe anajiita Ofisa wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma na kwamba amekuwa na tabia ya kuwalaghai watu na kuwadai fedha akisingizia kwamba atawasaidia kupata ajira ndani ya TAKUKURU na ofisi zingine za Serikali,” ilieleza taarifa.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba ufuatiliaji wao umeonesha mtuhumiwa
alimwahidi kaka wa mtoa taarifa wao kazi ya udereva ndani ya TAKUKURU na baada ya mtu huyo kumweleza kwamba hana leseni ya udereva daraja C, ndipo mtuhumiwa akataka apewe sh. 350,000 ili amsaidie kupata leseni.

“Baada ya kupokea taarifa hii na sisi tukaweka mtego na kumnasa
mtuhumiwa akiwa eneo la Kisasa Jijini Dodoma Aprili 14, mwaka huu,”
ilieleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo awali mtuhumiwa alimweleza mtoa taarifa wa TAKUKURU kwamba imetangaza nafasi nane za ajira ya madereva na kwakuwa nafasi nne zimeshachukuliwa, yeye atamsaidia mdogo wake kupata nafasi moja katika zile nafasi zilizosalia.

“Baada ya hapo tuliendelea na uchunguzi na kubaini kwamba mtuhumiwa alishawahi kujiita ofisa wa TAKUKURU Chamwino-Ikulu na kumtapeli rafiki wake wa kike ambaye alimtumia sh. 214,000 ili amsaidie dada yake kupata ajira Serikalini. Fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya mafaili na sare za kazi,”alisema na kuongeza;

“Ufuatiliaji zaidi ukatuwezesha kumbaini pia kijana mwingine, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambaye yeye na baba yake kwa pamoja wametapeliwa na Jumbe ambaye alijiita Afisa wa TAKUKURU wa Chamwino-Ikulu sh 2,452,500.”

Taarifa hiyo ilieleza kwamba fedha hizo zilitolewa ili awasaidie kumwezesha mwanafunzi huyo kupata ajira kama Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.

Mtuhumiwa alidai kupatiwa fedha hizo alizokuwa analipwa kidogo kidogo na kwamba zilikuwa ni kwa ajili ya gharama mbalimbali zikiwemo kufungua akaunti ya kupokelea mshahara, sare za kazi,  silaha na mafunzo ya kuitumia, matumizi wakati wa mafunzo, ukarabati wa nyumbaatakayoishi akianza kazi, tiketi ya ndege ya wazazi wake kwenda Dar es Salaam kushuhudia akiapishwa pamoja na kusafirisha gari atakalotumia kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.

TAKUKURU mkoa wa Dodoma ilisema inaendelea na uchunguzi dhidi ya
mtuhumiwa huyo ambaye wamebaini kwamba huwa anapokea fedha hizo za utapeli kwa njia ya simu au fedha taslimu na hatua stahiki
zitachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika.