Na Moses Ng’wat, TimesMajira Online, Songwe
WATU wawili wamefariki dunia papo hapo na mmoja kujeruhiwa Wilayani Mbozi, baada ya Lori la mizigo kupoteza mwelekeo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa lilifeli breki wakati likishuka katika mteremko wa Mlima Senjele ya pili katika barabara Kuu ya Tanzania – Zambia (Tanzam) na kuyagonga malori mengine mawili.
Akizungumzia kuhusu tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Malya, alisema tukio hilo lilitokea jana Aprili 6,2023 baada ya lori aina ya Scania lenye namba T 413 BAE na Trela lake T 444 BWF kufeli breki na kwenda kugonga malori mengine mawili na kusababisha vifo.
Alisema lori hilo lilokuwa likiendeshwa na dereva Peter Simwenda (39) , Mkazi wa Jijini Dae salaam ambaye kwa sasa amelazwa katika hospitali ya serikali ya Wilaya ya Mbozi, Mjini Vwawa baada ya kujeruhiwa vibaya, lilikuwa likitokea Tunduma kuelekea Jijini Dar es saalam.
Kamanda Malya alisema baada ya dereva huyo kushindwa kulimudu gari hilo alienda kuligonga Fuso lilokuwa mbele yake lenye namba za usajili T 418 AJR lilokuwa likitokea Wilaya ya Nkasi, Mkoani Rukwa kabla ya kuvamia Lori la mafuta lilokuwa likipanda mlima kutokea Mbeya lenye namba T957 CFT na trela lake namba T 513 BUS na kusababisha vifo vya watu wawili.
Aliwataja waliofariki kuwa ni utingo wa Fuso, Liberatus Mfaume (40) mkazi wa Nkasi Mkoani Rukwa na Ally Yusufu ambaye ni dereva wa Lori la Mafuta.
Hata hivyo, Kamanda Malya alitoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Songwe kuacha kukimbilia kuiba mali na badala yake wawewanatoa msaada kwenye matukio ya ajali.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu