January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Airtel, TADB waungana kuinua sekta ya kilimo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Dar es Salaam

KAMPUNI ya Simu ya Airtel, nchini Tanzania, imeungana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kwa kuingia makubaliano ya miaka mitatu, yenye lengo la kuinua na kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo kwa njia ya mtandao yaani- kidijitali.

Makubaliano ya ushirikiano huu kati ya Airtel Tanzania na TADB yanadhamira ya kufanikisha na kupanua ushirikiano wa sekta ya kifedha kwa wadau mbalimbali ndani ya sekta kilimo, wakiwemo wakulima na wajasiriamali wadogo vijijini, hususani wanawake na vijana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh (kushoto) akisaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Frank Nyabundege utakowawezesha wakulima wadogo. Wanaoshuhudia kitendo hicho ni (kutoka kushoto) Jemima Masimba, Meneja Miradi wa Airtel Tanzania, Juliana Kaswamila, Meneja wa Sheria na Udhibiti wa Airtel Money na Edson Rwechungura, Mtendaji wa Huduma za Kisheria wa TADB. Hafla hiyo ilifanyika Aprili 23, 2024 katika Makao Makuu ya Airtel Tanzania.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Jijini Dar es Salaam, Aprili 23, Mwaka huu, katika hafla ya kutiliana saini makubaliano hayo kati ya Airtel na TADB, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh, amesema.

“Airtel kwa kushirikiana na TADB tunadhamira ya dhati ya kusaidia Watanzania kupitia ubunifu katika sekta ya mawasiliano, hii ni kwakua tunaamini wakulima wanastahili kuwa miongoni mwa vikundi vinavyotakiwa kunufaika na ukuaji wa teknolojia nchini.

Hivyo, Ushirikiano wetu na TADB unalenga katika kutatua changamoto zinazowakabili wakulima kwa kutumia bidhaa mbalimbali za kidijitali, ambazo zitaibua masoko mapya kwa wakulima mijini na vijijini. Bidhaa hizo zitawezesha uzalishaji wa wakulima na kuongeza mapato yao”, amesema Balsingh.

Balsingh ameeleza kuwa, ushirikiano wa Airtel na TADB unaungana moja kwa moja na maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya ukuaji wa sekta ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege (katikati) wakibadilishana hati mara baada ya kusaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) unaolenga kuwainua wakulima wadogo nchini kote. Wanaosimama kando ni washiriki wa timu kutoka kampuni zote mbili.

“Na hii inaonesha jinsi kilimo kilivyo muhimu katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watu wamejiajiri katika sekta ya Kilimo”, ameeleza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji, Frank Nyabundege ameishukuru Airtel Tanzania na kusema kuwa, ushirikiano wa Airtel na TADB utafungua milango ya fursa katika sekta ya kilimo.

Pia amesema, ushirikiano huo utatoa fursa kwa wakulima kujipatia masuluhisho kwenye mahitaji na changamoto wanazokutana nazo katika shughuli zao za kila siku.

“Ubia wa Airtel na TADB unalenga kukuza ukuaji sekta ya kilimo, Ushirikiano huu ni mwanzo wa mabadiliko makubwa yatakayowagusa wakulima wote nchini Tanzania,” amesema Frank.

Aidha amesema, Ushirikiano huo pia unakwenda sambamba na mikakati ya Serikali ya kuunga mkono juhudi za wadau wa kilimo kwa kupambaa na changamoto mbalimbali ndani ya sekta ya kilimo, kwa kuwawezesha wakulima kifedha kama ilivyotajwa na Rais Samia, wakati wa mkutano wa wadau wa COP28 uliofanyika Disemba 4, 2023.

Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania (kushoto), Dinesh Balsingh akipeana mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege baada ya kusaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) hivi karibuni unaolenga kuwasaidia wadau wa kilimo. Tukio hilo lilifanyika Aprili 23, 2024 katika Makao Makuu ya Airtel Tanzania.