Na Mwandishi wetu, TimesmajiraOnline,Mbeya
IMEELEZWA kuwa wanawake wanapaswa kupata haki zote na kuwa wanufaika katika nyanja mbalimbali, ikiwemo uchumi, ili kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza katika jamii.
Kauli hiyo imetolewa Machi 6, 2026 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Aida Haule, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Wanawake yaliyofanyika katika eneo la Tarafani, Mji wa Mbalizi wilayani Mbeya. Katika hafla hiyo, Mhe. Haule alikuwa mgeni rasmi na alisisitiza kuwa msingi wa maendeleo ya jamii ni kuhakikisha haki zinatolewa kwa usawa katika nyanja zote.
“Mwanamke anapopata haki zote, inasaidia kuondoa vizuizi vya kimfumo na kumwezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi,” amesema Haule.

Awali akisoma risala kwa niaba ya Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Agness Elikunda, Afisa Maendeleo ya Jamii Gift Kayunguya alisema wanawake hawapaswi kuachwa nyuma katika harakati za maendeleo.
Aidha, Kayunguya amesema haki jumuishi kwa wanawake na wasichana ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu, kwani huwasaidia kupata usawa wa kijinsia na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
“Wanawake wakipata haki sawa, inasaidia kuondoa vikwazo vinavyowazuia kujihusisha na shughuli za kiuchumi, jambo ambalo ni muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050,” amesema Kayunguya.
Kwa upande wake, Tabia Sadick, mkazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, akizungumza na Timesmajira Online, ameishukuru Serikali kwa juhudi zake za kuwasaidia wananchi, lakini akaomba kuangaliwa zaidi suala la ajira kwa wasichana waliomaliza elimu ya juu.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kutuwezesha kusomesha watoto wetu, lakini changamoto iliyopo ni ukosefu wa ajira kwa watoto wa kike. Wakipata ajira itasaidia kuepuka vishawishi vinavyoweza kuwakumba,” amesema Tabia.
Naye Felista Mwangonela, mkazi wa eneo hilo, amesema kikundi chao cha wanawake kimenufaika na mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri, ambapo waliutumia mkopo huo kununua mazao na kuyauza ili kuongeza kipato.
Maadhimisho ya Wiki ya Wanawake Duniani hufanyika kila mwaka ifikapo Machi 8. Hata hivyo, baadhi ya halmashauri zimeanza maadhimisho hayo mapema. Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: “Haki kwa wanawake na wasichana ni msingi wa maendeleo jumuishi kufikia Dira ya Maendeleo 2050.”


More Stories
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
LGTI wanawake waadhimisha siku yao Ngorongoro
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi