Mwandishi: Ismail Mayumba
Email ni moja ya njia muhimu ya mawasiliano ya kidigitali inayotumiwa sana na Watanzania. Iwe kwa matumizi binafsi, ya kiofisi au ya kiserikali, email inachukuliwa kama njia rasmi zaidi ya kuwasiliana kuliko sms au WhatsApp. Huduma kama za RITA na NIDA zinahitaji mtu awe na akaunti ya email ili aweze kupata huduma zao kupitia mifumo yao ya mtandaoni. Hii imewalazimu hata wananchi wa kawaida kuwa na email.
Kutokana na umuhimu huu, wahalifu wa kimtandao wameanza kuelekeza mashambulizi yao kwenye akaunti za email kwa sababu wanajua humo ndimo taarifa nyeti zinapatikana. Ili kupambana na hali hii, kampuni kama Google zimeweka mifumo ya kuchuja barua pepe hatarishi kwa kutumia teknolojia inayoitwa spam filter. Hii ni teknolojia inayotambua na kuzuia email zinazodhaniwa kuwa na madhara.
Awali, spam filter ilitegemea zaidi orodha ya maneno hatarishi au anwani za email ambazo mtumiaji mwenyewe amezizuia. Ila baadaye, waliona hiyo haitoshi. Teknolojia ikaongezewa uwezo wa akili bandia na ikawa inajulikana kama AI spam filter. Hii inatumia akili bandia kuchambua tabia ya email bila ya kutegemea tu maneno au orodha ya anwani zilizozuiwa. Inatambua kwa undani aina ya maudhui, viambatisho na tabia ya kutuma ili kubaini kama email ni salama au la.
AI spam filter imekuwa msaada mkubwa katika kupunguza uhalifu mtandaoni. Imeweza kuondoa barua pepe nyingi hatarishi kabla hazijafika kwa watumiaji, hivyo kusaidia kulinda taarifa na data zao binafsi.
Hata hivyo, kuna changamoto. Wakati mwingine AI spam filter inaweza kusema email nzuri ni hatarishi na kuizuia (false positive) au inaweza kuruhusu email hatarishi kuingia kama salama (false negative). Changamoto hizi zinahitaji uelewa mzuri ili kuziepuka.
Njia bora ya kulinda taarifa zako ni kuangalia folder la spam kabla ya kufuta email zote. Mara nyingi watu hupoteza email muhimu kwa sababu hawakufuatilia vizuri spam folder. Tofauti ni kwamba, ukifuta email kutoka spam zinafutika moja kwa moja bila kuingia kwenye trash. Lakini email kutoka inbox huenda kwenye trash na hukaa kwa muda wa siku 30 kabla ya kufutwa kabisa. Hii inakupa nafasi ya kubadilisha maamuzi kama kuna kilichokosewa.
Kwa hiyo, kabla hujaamua kufuta email zote kwenye spam, ni vyema kupitia moja baada ya nyingine. Kama kuna email uliyokuwa ukitegemea lakini hujaiona kwenye inbox, hakikisha unaangalia pia kwenye spam. Kama ipo, chukua hatua sahihi kama kuifungua au kuwasiliana na aliyekutumia.
AI spam filter ni teknolojia ya kisasa yenye manufaa makubwa, lakini pia ina mapungufu. Kuielewa na kujua namna ya kuitumia kwa usahihi ni hatua muhimu ya kulinda taarifa zako binafsi na za ofisi. Usalama wa data ni jukumu la kila mmoja wetu.
More Stories
TAKUKURU yanasa watuhumiwa wa wizi wa mali za wakulima
CCM yampongeza Rais Samia kutunukiwa tuzo na Bunge
Mwenge wazindua Miradi saba Temeke