January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ahukumiwa miaka 30 kwa kukutwa na dawa za kulevya

Na Grace Gurisha

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi, imemuhukumu, Said Malikita kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na dawa za kulevya gramu 238.24 aina ya heroin hydrochloride.

Hukumu hiyo imesomwa na Jaji Lilian Mashaka wa Mahakama hiyo, ambapo amesema upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shtaka hilo bila kuacha shaka lolote.

Jaji Mashaka amefikia uamuzi huo ni baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi nane wa upande wa mashtaka, vielelezo vitano na kupitia sheria mbalimbali ambazo zinahusiana na makosa ya dawa za kulevya.

“Baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, wameweza kuthibitisha kesi inayomkabili, Malikitika bila kuacha shaka lolote, Mahakama imemkuta na hatia ya kosa la kukutwa dawa za kulevya, kwa hiyo atatumikia kifungo cha miaka 30 jela,” alisema Jaji Mashtaka.

Kabla ya Jaji Mashaka kusoma hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Costantine Kakula akisaidiana na Wakili wa Serikali Baltrida Mushi waliiomba Mahakama hiyo itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine na jamii kwa ujumla.

Said Malikita akiwa amesindikizwa na askari Magereza.

Hata hivyo walisema hilo ni kosa lake la kwanza. Baada ya Wakili Kakula kudai hivyo, mshtakiwa Malikita alivyopewa nafasi ya kuomba kupunguziwa adhabu alisema kuwa ni kosa lake la kwanza, baba na mama yake ni wazee sana na pia tangu akamatwe na kuwekwa gerezani hajawahi kuonana na mama yake.

Pia, amesema ana watoto wawili, ambao wanamtegemea yeye na kwa sasa hawana ada za shule, kwa hiyo anaiomba Mahakama impunguzie adhabu.

Mshtakiwa Malikita alikuwa akitetewa na Wakili Abraham Senguji. Mshtakiwa Malikita alikamatwa Agosti 29, 2017 katika Mtaa wa Ufipa, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam akiwa na dawa za kulevya gram 238.24 aina ya heroin hydrochloride.