January 27, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ahukumiwa kifungo jela kwa kumtusi mama yake mzazi

Na Grace Gurisha,TimesMajira,Online, Dar

MAHAKAMA ya Wilaya Ilala imemuhukumu mfanyabiashara, Zarina Sidik kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kupatikana na makosa ya kumtukana matusi ya nguoni mama yake mzazi.

Hukumu hiyo imesomwa jana (Agosti 26,2021) na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Martha Mpaze, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wa nne wa upande wa mashtaka ukiwemo ushahidi wa mama yake mzazi, Rafika Hawa Sidik.

Amesema kutokana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka umetbibitisha shtaka bila kuacha shaka.

“Kwa hiyo Mahakama inamtia hatiani kwa kosa aliloshtakiwa nalo la kutoa lugha chafu,” amesema hakimu.

Hakimu Mpaze amesema amezingatia hoja za pande zote mbili na ameona mshtakiwa ni mkosaji wa mara kwa mara, ambapo angekuwa ni wakubadilika alivyotiwa hatiani asingerudia makosa.

“Ili iwe fundisho kwako na kwa wengine wanaotukana wazazi wao, Mahakama inakuhukumu kwenda jela mwaka mmoja gerezani,” amesema Hakimu Mpaze. Kabla ya Hakimu Mpaze, kutoa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Nancy Mushumbusi aliomba mshtakiwa apewe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine kwani ni mkosaji anayerudia makosa.

Wakili Nancy amedai mshtakiwa amewahi kutiwa hatiani mara mbili katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo kwa makosa kama hayo akaonywa na sasa hivi ana kesi nyingine inaendelea katika Mahakama ya Mwanzo Ukonga.

Amedai apewe adhabu kali kwani ameenda kinyume na mila na desturi  za kitanzania ,kamtukana mama yake mzazi ambaye alitoa ushahidi kwa uchungu huku akilia.

Baada ya Wakili Mushumbusi kudai hivyo naye mshtakiwa Zarina alipewa nafasi ya kujitetea ili apunguziwe adhabu na Mahakama kwa sababu tayari ilishamtia hatiani kwa kosaa hilo.

Zarina aliomba apunguziwe adhabu,  alidai kuwa yeye ni mama mwenye watoto wanamtegemea, hajaolewa na anapitia changamoto nyingi za kisaikolojia.

Pia, anadai hakumtukana mama yake na kudai kesi hiyo ilitokana na masuala ya biashara na kwamba wanataka aondoke katika familia.

Pia, Zarina aliomba apewe nafasi nyingine atajirekebisha. Mshtakiwa huyo katika utetezi wake alikuwa na mashahidi watatu waliomtetea yeye, ambapo utetezi wao haukuweza kuepusha na kifungo cha mwaka mmoja jela.

Ilidaiwa kuwa Novemba 29, 2019, Zarina akiwa eneo la Kariakoo Uhuru Nyamwezi ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam alimtolea mama yake kwa ambayo kwa misingi ya kimaadili tumeshindwa kuyachapisha.