Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoani Tabora imemuhumu Adamu Frank Kipasile (31) dereva, mkazi wa Moshi Mkoani Kilimanjaro kwenda jela miaka 20 au kulipa faini ya sh mil 20 baada ya kumtia hatiani kwa kosa la usafirishaji haramu wa binadamu kinyume cha sheria.
Akitoa hukumu hiyo juzi Hakimu Mkazi Gabriel Ngaeje alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya gari alilokuwa akisafirishia raia 3 wa Kisomali kupata ajali na kupinduka katika kijiji cha Makomero Wilayani Igunga Mkoani hapa.
Akitoa hukumu ya kesi hiyo Hakimu Ngaeje alisema mahakama imemtia hatia mshitakiwa kwa kosa la kusafirisha binadamu raia 3 wa Kisomali ambao ni Abdullah Mohamed 28, Zakaria Zekele 18 na Deka Haile 27 kinyume cha sheria za nchi.
Dereva huyo alikuwa akiendesha gari yenye namba ya usajili T 711 CPC aina ya Toyota Wish iliyokuwa ikitokea Moshi kwenda Tabora na kuacha njia kisha kupinduka na raia hao kupata majeraha na kupelekwa hospitali ya Wilaya kwa ajili ya matibabu.
Hakimu Ngaeje alisema raia hao tayari wamerudishwa kwao baada ya kulipa faini ya sh laki 5 kila mmoja kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.
Wakili wa Uhamiaji Octavian Kilatu aliiambia Mahakama kuwa raia hao walikuwa wakisafirishwa kinyume cha utaratibu wa sheria za uhamiaji ambapo dereva Adamu alikamatwa kwa kosa hilo majira ya jioni.
Wakili huyo aliiambia mahakama kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi ambao ulisababisha kupata ajali na kupinduka ndipo raia wema walitoa taarifa.
Raia hao kutoka nchini Somalia walikiri kufanya kosa hilo na kutozwa faini ya laki 5 kila mmoja na ndugu zao walifika mahakamani hapo na kutoa fedha hizo, hivyo kurudishwa kwao.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua