September 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Agizo la Rais Dkt. Samial awakuna maaskofu TEC

*Nao waungana naye wakitaka uchunguzi haraka, wataka watakaobainika kushindwa kuwajibika, wawajibishwe, hawaamini kama makundi hayo ya kihalifu yana nguvu

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Dar

BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa kauli inayoonesha kuungana na Rais Samia Suluhu Hassan, aliyeagiza kufanyika uchunguzi haraka na kupelekewa taarifa ya wale wote waliohusika na matukio utekaji na mauaji.

“Tunaunga mkono wito wa viongozi na watu mbalimbali wa kufanyika uchunguzi wa kina na haraka ili wale wote waliohusika na matukio hayo yafikishwe mbele ya sheria.”

Ujumbe TEC uliotolewa jana katika Kilele cha Kongamano la Tano la Ekaristi Takatifu la Kanisa Katoliki lililofanyika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam ambapo ulisomwa na Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa.

Ingawa Askofu Nzigilwa hakumtaja Rais Samia moja kwa moja, lakini baada ya kutekwa na kupatikana kiongozi wa CHADEMA, Ali Kibao, akiwa ameuawa Rais Samia, aliagiza vyombo vya uchunguzi kumpelekea taarifa ya mauaji ya kiongozi huyo na matukio mengine haraka.

Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa Septemba 8,2024 katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Rais Samia alitoa maelekezo hayo akieleza kusikitishwa kwa tukio hilo.

“Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya mauaji ya kiongozi wa CHADEMA, bwana Mohamed Ali Kibao. Natoa pole kwa viongozi wa chama hicho, familia ya Mzee Kibao, ndugu, jamaa na marafiki,”

“Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna.”

Askofu Nzigilwa alisema kauli mbiu ya kongamano hilo ni ‘Udugu huponya ulimwengu, sisi sote ni ndugu.’ Alisema kwa miaka mingi Tanzania imekuwa inasifika kama kisiwa cha amani licha ya tofauti za kidini, kikabila na kiitikadi bado umoja ulitawala, lakini kwa hali ilivyo sasa inakwenda tofauti.

“Matukio yaliyotokea karibuni ya watu kutekwa na hata kuuawa, tunajiuliza nini kimetokea, Taifa letu limekosea wapi je, uongozi na mamlaka husika na vyombo vya ulinzi na usalama vimezidiwa nguvu na maarifa hadi kushindwa kudhibiti hali hii?

Sisi maaskofu hatuamini kama makundi haya ya kihalifu yana nguvu kuliko vyombo vyetu ya ulinzi na usalama. Hivyo tunaviomba vyombo kutimiza wajibu wake ili kurudisha heshima yetu ya misingi ya udugu na amani,” alisema.

Alizidi kusema kwamba; “Tunaungana na watu, taasisi, jumuiya za kimataifa kulaani na kukemea vitendo hivi vya kihalifu na utekaji, tunaunga mkono wito wa viongozi na watu mbalimbali wa kufanyika uchunguzi wa kina na wa haraka ili wale wote waliohusika na matukio hayo wafikishwe mbele ya sheria.

Aidha, kupitia ujumbe maaskofu hao uliosemwa na Askofu Nzigilwa walitaka ambao hawakuwajibika kwa kadri ya nafasi zao wawajibishwe.

Alisema uhai ni zawadi kutoka kwa Mungu, mtu ameumbwa kwa sura na mfano wake mwenyewe. “Maisha na utu wa mtu lazima viheshimiwe na kulindwa kwa nguvu zote,” alisisitiza.

Alisema wanapoangalia Taifa la Tanzania limejulikana duniani kama kisiwa cha amani na mahali pekee Afrika ambapo raia wake mbali na tofauti zao za kikabila, kiimani , kiitikadi, na kiuchumi, wameweza kuishi kwa umoja, kiimani na kiundugu.

Alisema kila mtu alihakikisha anaiishi tumu hiyo na kuilinda . “Lakini tukiangalia hali ya sasa tunaona tundu tunu yetu imeshambuliwa kutokana na matukio yaliyotokea siku za karibuni na watu kutekwa, kuumizwa na hata kuuawa.