December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwendesha pikipiki akipita katika kundi la Nzige wa Jangwani katika kaunti ya Isiolo, nchini Kenya. Picha ya AP

Afrika Mashariki kukumbwa na nzige tena

ROME, Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) limebainisha kuwa, wimbi la pili la nzige wa jangwani linatarajiwa kusababisha uharibifu mkubwa Mashariki mwa Afrika.

Hali hiyo itajitokeza ikiwa ni miezi miwili baada ya kundi la wadudu hao hatari kuvamia mimea siku chache kabla ya kuanza kwa mlipuko wa virusi vya Corona.

Aidha, uvamizi huo unatajwa unahatarisha kusababisha tatizo la chakula ambalo tayari limekuwa likitarajiwa katika Pembe ya Afrika.

Nzige wa jangwani tayari wamevamia nchini Somalia, Ethiopia, Kenya, Uganda, Ethiopia na Sudan Kusini mara moja mwaka huu, mwezi Januari na Februari.

”Mara ya mwisho Kenya kuathiriwa na uvamizi wa nzige wa kiwango kama hiki ni miaka 70 iliyopita wakati ilipokuwa chini ya ukoloni wa Uingereza,”alisema Keith Cressma, mtaalamu wa utabiri wa nzige katika Shirika la FAO.

Hivi karibuni, FAO llitangaza kuwa, linaendelea na juhudi zake kwa kushirikiana na nchi athirika kwa ajili ya kudhibiti baa la nzige wa jangwani katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki licha ya kuweko vizingiti vya kusafiri watendaji wake na kusafirisha vifaa kutokana na mlipuko wa virusi vya corona (COVID-19).

Shirika hilo la FAO lilisisitiza kuwa, hali ya mlipuko wa nzige wa jangwani bado ni mbaya katika nchi za Pembe ya Afrika na kwamba inahatarisha usalama wa chakula hususan katika nchi za Ethiopia, Uganda, Somalia na Kenya.

Baadhi ya ripoti zinaeleza kuwa, kwa sasa madhara ya nzige hao ni makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 25 iliyopita kwenye eneo la Afrika Mashariki na Asia Kusini.

”Inaonekana kwamba wale waliokwepa Covid-19 watakabiliana na Locust 19,”, alisema Akiwumi Adesina Mkuu wa Benki ya Maendeleo barani Afrika na Waziri wa zamani wa Kilimo wa Nigeria.