March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afisa Tarafa Chipanga akemea watumishi kufanya kazi kwa mazoea

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Bahi

AFISA Tarafa ya Chipanga Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma, Chrstian Kiiza amewataka watendaji wote waliopo ndani ya tarafa hiyo kuhakikisha wanafanya kazi kwa kufuata misingi ya kazi kwa mujibu wa Sheria,Kanuni na taratibu ikiwa ni pamoja na kuzingatia mipaka yao ya kazi.

Kiongozi huyo ametao kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na Watendaji pamoja na wafugaji ambao walikuwa na malalamiko ya kuonewa na ofisi ya kijiji.

Akizungumza na watendaji amesema kuwa kila mtumishi anatakiwa kutambua wajibu wake kwa kufanya kazi kwa kufuata misingi ya kazi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kutumia ofisi za Serikali vibaya.

Kiiza amesema kuwa ni wajibu wa kila mtumishi kutambua umuhimu wa kufanya kazi yake kwa kuzingatia misingi ya kazi na kuelewa kuwa anafanya hivyo kwa kuwatendea watu wote haki bila ya upendeleo wowote.

“Watumishi wa serikali mnapokuwa kazini ni lazima mkatambua kuwa mpo kazini kwa ajili ya kuhudumia jamii inayowazunguka na kwa kutenda haki ikiwa ni pamoja na kila mmoja kutambua mipaka ya utendaji wa kazi.

“Kila mmoja afanye kazi kwa kutambua mipaka yake ya kazi,kutumia utaalamu wake kuwasaidia watu ambao wanatakiwa kuwasaidia ikiwa ni pamoja kupawatia maelezo ambayo yanaambatana na utoaji wa elimu ya mambo ambayo yanahitaji kutolewa elimu.

“Watendaji na watumishi wa Umma mnatengeneza migogoro kati ya wananchi na Serikali kutokana na kutofuata misingi ya utendaji kazi na kuingilia majukumu ambayo wakati mwingine siyo ya kwenu kwa kutokujua mipaka ya kazi au kufanya kazi kwa mazoea jambo ambalo siyo sahihi katika kufanya kazi ya kuhudumia jamii”amesema Afisa Tarafa Kiiza.

Katika hatua nyingine amewataka hata wana siasa kufanya kazi kwa lengo la kusimamia maendeleo ya wananchi waliowachagua na kuachana na tabia ya kujenga matabaka au kutengeneza migogoro kwa nia ya kujitengenezea faida.