Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilayani Igunga Mkoani Tabora imemkamata na kumfikisha mahakamani aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Wilayani Igunga (IGUWASA) Husseni Salumu Nyemba (34) kwa tuhuma za uhujumu uchumi.
Awali Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU kutoka Wilayani Nzega, Mazengo Joseph akisoma shitaka linalomkabili mtuhumiwa huyo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Igunga Lydia Ilunda alisema mtuhumiwa alitenda kosa hilo Julai 2021na amefunguliwa kesi na.1/2023.
Aliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo akiwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji (IGUWASA) katika kabla ya kuhamishiwa Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi kushika nafasi kama hiyo hiyo kwenye Mamlaka ya Maji.
Mazengo alingeza kuwa mtuhumiwa anakabiliwa na shitaka la uhujumu uchumi la kujipatia manufaa kwa njia zisizo halali kinyume na kifungu cha 23 (1) (a) na (2) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa cha 329 mapitio ya 2019 ikisomwa pamoja na sheria ya uhujumu uchumi.
Alisema mtuhumiwa alijipatia kiasi cha mil 4 kutoka kwa mfanyabiashara wa Jijini Dar es salaam, Rashidi Mwinyimkuu Mbegu ambaye alikuwa anadai malipo yake baada ya kutoa huduma ya vifaa katika mamlaka hiyo ambapo kiasi hicho kilitolewa ili kulipwa fedha zake anazodai IGUWASA.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo mtuhumiwa alikana kutenda kosa hilo na kesi imeahirishwa hadi Mei 16, 2023 kwa ajili ya kusikiliza hoja za awali baada ya upande wa Jamhuri kusema uchunguzi wa kesi hiyo umekamilika, mshtakiwa yupo nje kwa dhamana ya sh mil 2.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili