December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afikishwa Mahakamani kwa tuhuma za ulawiti, 241 wahukumiwa vifungo jela kwa makosa ya ukatili

Na.l Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka baada limemfikisha mahakamani mkazi mmoja (46) wa Sombetini Jijini Arusha kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wake ambaye jina lake limehifadhiwa umri miaka saba mwanafunzi wa darasa la kwanza jijini humo.

Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo amesema pamoja na kuwepo kwa tukio hilo pia kwa kipindi cha mwezi Januari mwaka jana  hadi Januari mwaka huu jumla ya watuhumiwa 241 walipatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda jela  vifungo mbalimbali  kwa makosa ya ulawiti na ubakaji.

Aidha alibainisha kuwa februari 16, 2023 Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilimhukumu mtu mmoja aitwaye KELVIN WILFRED (19) mkazi wa Muriet Arusha kwenda Jela kifungo cha Maisha kwa kosa la kumbaka mwanafunzi amabaye jina lake limehifadhiwa umri miaka nane wa darasa la Nne.

Sambamba na hilo amesema Mahakama ya wilaya ya Karatu, Arumeru na Monduli ziliwahukumu PETER LEONARD  (27) mkazi wa Lashaine Monduli, PAUL HILONGA (60) mkazi wa Karatu, JOHN SANARE (24) mkazi wa Arumeru kwenda Jela vifungo vya maisha kila mmoja  kwa makosa ya Ubakaji na ELIASI NDASIKOI (23) mkazi wa Arumeru naye alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la Kulawiti.

Ameendelea kufafanua kuwa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru na Karatu  vifungo vya miaka 30 kila mmoja kwa makosa ya ubakaji ni JAMES ELIREHEMA mkazi wa Maloloni ELIAS ROBERT (27) mkazi wa Ambureni, JAPHET MUNGURE wote wa wilaya ya Arumeru  na  THEOPHILI SALAHO (32) mkazi wa kijiji cha Chanoldean wilayani Karatu.

Aidha amesema jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya serikali litaendelea kufuatilia kwa mujibu wa sheria wale wote watakaobainika kutenda matukio ya uhalifu ikiwemo ya ukatili na unyanyasaji katika jamii.

ACP Masejo amesema kuwa Jeshi hilo linawashukuru wadau mbalimbali ikiwemo wazazi, viongozi wa Dini, viongozi wa kimila na Waandishi wa Habari kupitia dhana nzima ya ushirikishwaji wa jamii ambayo imepekelekea jamii kuacha kuficha matukio ya ukatili badala yake wanayaibua na kuripoti matukio mengi yanayotokea.

jeshi hilo la polisi limetoa wito kwa wazazi na walezi, viongozi wa dini, mila, serikali pamoja na wadau wengine kuendelea kutoa elimu pamoja na kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili katika jamii ambao unapelekea kuongezeka kwa matukio hayo.
 
Wawili wafariki dunia kwa ajali ya pikipiki, wanne wajeruhiwa.

Katika tukio jingine ACP Masejo amesema februari 15, 2023 muda wa saa 01:00 jioni huko maeneo ya Momela, Wilaya ya Arumeru katika Barabara ya Moshi – Arusha gari lenye namba za usajili T. 493 BJR aina ya Corona Premio likiendeshwa na Dereva aitwaye ALLY IDD (45) mkazi wa Maji ya Chai liligongana na pikipiki ikiendeshwa na dereva aitwaye ELISHA ANTHONY iliyokuwa imepakia watu watatu na kusababisha vifo kwa watu wawili pamoja na majeruhi wanne ambapo katika ajali hiyo pikipiki mbili zilihusika.

Kamanda Masejo amewataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni ELISHA ANTHONY (25) Dereva pikipiki pamoja na PIUS CALIST TARIMO (17) dereva wote wakiwa ni wakazi wa Sokoni One Jijini Arusha.
Aidha waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni PAULO HENRY (20) mkazi wa Sokoni One, SAIDI ELIAS (23) mkazi wa Uswahilini walipatiwa matibabu na kuruhusiwa. 

Aliendelea kuwataja majeruhi wengine kuwa ni EMMANUEL JOHN (18) mkazi wa Uswahilini na Joshua Fredy Laizer (23) mkazi wa Levolosi ambao wanaendelea kupatiwa matibu katika Hospitali ya Mount Meru Arusha.

ACP Masejo amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa pikipiki ambazo zilikuwa zinatokea Moshi kwenda Arusha, wakati zikiyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari na kupelekea kwenda kugongana na gari hilo.

Mwisho amesema kuwa jeshi hilo linaendelea kutoa wito kwa madereva wote pamoja na watumiaji wa vyombo vya moto kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea kutokana na ajali.

Pia amesema wataendelea kutoa elimu na kuchukua hatua kali za kisheria kwa madereva wote wazembe ikiwemo kuwafungia leseni zao na kuwafikisha mahakamani ili hatua zaidi zichukuliwe dhidi yao.