Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online-Rukwa
Mwanamke aliyefahamika kwa jina la Magreth Chakupewa (26) mkazi wa kijiji cha Kate Kata ya Kate wilayani Nkasi mkoani Rukwa,amefariki baada ya kupigwa na radi.
Shuhuda wa tukio hilo Crisence Kwimba amesema Jumamosi majira ya saa 11 jioni wakati mwanamke huyo alipokuwa ametoka shambani akiwa ameambatana na mwenzake baada ya muda radi ilitua na kumpigia Magreth.
Lakini mwenzie alisalimika na kukimbilia kijijini kwenda kutoa taarifa juu ya tukio hilo.
Baba wa marehemu Joseph Chakupewa amedai kuwa mtoto wake huyo alitoka asubuhi kuelekea shambani anakojishughulisha na kilimo cha mahindi lakini jioni alishitushwa na taarifa za kifo hicho kilichotokana na radi.
Amedai kuwa mtoto wake huyo hadi mauti yanamkuta ameacha mtoto mdogo wa kike wa mwaka mmoja na miezi 7.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kate,Victor Chang’a,amekiri kutokea kwa changamoto hiyo na kuwa taratibu zote za kiserikali zimefanyika na kujiridhisha kuwa kifo hicho kimetokana na radi.
Amesema kuwa eneo hilo la Kate limekuwa na matukio ya mara kwa mara ya radi na kuwa ipo haja ya elimu kutolewa juu ya kukabiliana na matukio hayo ya mara kwa mara.
Mkuu wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua kwa kufuata maelekezo ya wataalamu ya namna ya kujikinga na majanga mbalimbali ikiwemo ya radi.

More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani