November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ADC: Queen Sendiga ni hazina ya nchi hii

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

CHAMA cha Alliance For Democrat Change ADC kimetoa wito kwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kumtumia vema mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Cuthbert Sendiga kikiamini ni hazina ya nchi hii.

ADC imeeleza kuwa ndani ya muda mfupi aliyotumikia umma ameonesha kuwa ni kiongozi shupavu mwenye maono ya mbali ambaye pia hayumbishwi.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu mkuu wa ADC, Doyo Hassan Doyo alisema uthubutu wake na namna anavyojenga hoja za kimaendeleo,ni msaada mkubwa sana kwa serikali.

“Mkoa wa Manyara umepata kiongozi shupavu naamini kwa uwezo wake,weledi na uchapakazi wake atawafikisha mbali wananchi wa Manyara ” alisema Doyo.

Hata hivyo Doyo aliongeza kusema kwamba sera na falsafa zake ambazo alizinadi mwaka 2020 akiwa mgombea wao katika kiti cha Urais,anazitekeleza Kwa vitendo na ndizo zilizomtambulisha Kwa muda mfupi katika Siasa za nchi hii.

“Mwaka 2020 tulimpa dhamana Queen agombee kiti cha Urais,falsafa zake za kuamini katika maendeleo ya jamii,kupambania usawa wa kijinsia,kutaka kuwakomboa watanzania kupitia kilimo,elimu na afya ndizo anazozitekeleza Kwa kiasi kikubwa mkoani Manyara “

“Tumeshuhudia jinsi anavyosimamia mabilioni ya fedha za umma katika elimu, miundombinu ya barabara na anavyowavutia wawekezaji kuingia mkoani Manyara,ni wazi mwanamama huyu ni hazina kwa Taifa letu” ameongeza Doyo.

Aidha Doyo ameeleza kwamba hata baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, viongozi walioingia madarakani walivutiwa na siasa zake na ndiyo siri iliyozidi kumtangaza Queen Sendiga katika ulingo wa siasa hadi leo hii.

Doyo anaamnini maono ya mwanasiasa huyo ambaye kwasasa ni mkuu wa Mkoa wa Manyara yatalifikisha Taifa hili katika mafanikio makubwa endapo ataendelea kuaminiwa na viongozi wa juu.

Amaebainisha kuwa kutokana na kwamba Queen Sendiga ni mpenda ukweli na ni mkweli asiyeyumbishwa katika kazi anapaswa kulindwa na kuaminiwa zaidi.

Doyo alisema ADC inajivunia kuwa na kiongozi wa serikali aliyetokana na chama chao na hili limekipambanua chama chao kuwa na viongozi waadilifu na wachapa kazi.

Queen Sendiga aliwahi kukitumikia chama Cha ADC kama Naibu Katibu mkuu ngazi ya Taifa

Kadhalika Mnamo Mei 15,2021 Queen Cuthbert Sendiga aliteuliwa Kwa mara ya kwanza kuwa mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Hata hivyo Julai 28,2022 alihamishiwa mkoani Rukwa ambapo kwasasa anautumikia mkoa wa Manyara.