Na Mwandishi Wetu, TimesMajira
PATRON wa ‘Kabaddi Sports Tanzania’ Adarsh K. Sharma atembelea kambi ya timu ya Taifa ya Tanzania ya mchezo wa Kabaddi iliyoingia kambini wiki iliyopita kujiandaa na mashindano ya Kabaddi Afrika ‘Africa Kabaddi Championship 2021’ yatakayofanyika hapa nchini.
Tayari wachezaji 34 Wanawake na Wanaume wameingia kambini katika hosteli za Juhudi katikati mwa wiki iliyopita ili kuanza kujiandaa na mashindano hayo na kuhakikisha ubingwa unabaki hapa nchini.
Kambi hiyo ya awali ya timu ya Taifa imefadhiliwa na Kampuni ya Demeter ‘Demeter Insurance Company Ltd’ pamoja na Pangani Pure Drinking Water kabla ya baadaye kuingia rasmi kufanya maandalizi ya mwisho kuelekea kwenye mashindano hayo ya Afrika.
Nyota hao watachuana na timu kutoka nchini Kenya, Cameroon, Egypt, Mauritius, Sirra Leone, Uganda, Afrika Kusini, Nigeria na Zimbabwe.
Mwenyekiti wa Chama cha Mchezo cha Kabaddi Tanzania (TKSA) Abdallah Nyoni amesema kuwa, Patroni Adarsh K. Sharma ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Demeter Insurance Company Ltd alitembelea kambi hiyo ili kuangalia maendeleo ya wachezaji.
Amesema, kiongozi huyo ambaye ni mfadhili wa kambi hiyo akishirikiana na Mr. Munawar wa Maji ya Pangani, ameridhishwa na maendeleo na kuahidi kujitolea zaidi kwa wachezaji ambao wanafanya mazoezi katika Uwanja wa Uhuru kila siku asubuhi na jioni.
Kiongozi huyo amesema kuwa, kwa sasa wanaangali ni namna gani wataweza kupata wafadhili wengine ambao wataisadia timu kupata mahitaji mengine kwani bado timu ina mahitaji mengi ili kufanya kambi hiyo kuwa na manufaa.
“Tunamshukuru Patroni wetu Adarsh K. Sharma kwa kutembelea kambi na kutupa matumaini makubwa katika maandalizi yetu lakini pia tunaomba wadau wengine wajitokeze kusaidia timu hii kwa chakula, posho za wachezaji na mishaanda mingine ambayo inaweza kupitia kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam ambao ni waratibu wa Mashindano Afrika,” amesema Nyoni.
Awali timu hiyo ilitakiwa kuingia kambini mwanzoni mwa mwezi uliopita chini ya makocha wa kimataifa wa mchezo wa Kabaddi kutoka nchini India, Amrik Singh na Vijender Singh ambao wangeshirikiana na makocha wa hapa nchini.
Lakini kabla ya makocha hao kutua hapa nchini kwa ajili ya mashindano hayo yaliyopangwa kuanda Desemba 11 hadi 15, Africa Kabaddi walitangaza kuyaahirisha kutokana na baadhi ya nchi kushindwa kuthibitisha kutokana na kuendelea kukabiliwa na ugonjwa wa Corona.
Licha ya mashindano hayo kuahirisha lakini nchi wanachama zitakazoshiriki mashindano hayo zimetakiwa kuwasilisha majina na nakala za hati ya kusafiria za wajumbe wao kabla ya Desemba 31, 2020.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania