November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ACT yaitaka Serikali kuchukua hatua uhaba wa walimu

Na Penina Malundo,timesmajira,Online

CHAMA   cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuchukua hatua kupunguza  changamoto sugu ya uhaba wa walimu kwenye shule shikizi nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu kwenye Kata ya Mpepai Jimbo la Mbinga Mjini inayoongozwa na Diwani wa ACT Wazalendo Donatus Donatus Mbepera.

Akikagua ujenzi wa madarasa katika Shule Shikizi ya Mwamko,  Ado amempongeza Diwani Mbepera kwa kusimamia vizuri miradi ya elimu, afya na maji katika Kata yake na kutoa  rai kwa Serikali kuhakikisha Shule Shikizi zinapatiwa walimu zaidi ili kuwapunguzuia mzigo walimu wachache waliopo.

“Tumefarijika na jitihada zilizochukuliwa kwenye ujenzi wa madarasa lakini, bado kuna uhaba mkubwa wa walimu, Mathalani, hapa Shule Shikizi ya Mwamko, kuna Mwalimu Mmoja tu anayefundisha Wanafunzi 187. Hili tunalichukua na tutalifikisha Serikalini,” amesema  Ado.

Akiwa katika Shule ya Sekondari ya Ali Mohamed Shein, Ado amesema kuwa falsafa ya Chama cha ACT Wazalendo ni “Siasa ni Maendeleo” na Chama kinaitekeleza kwa vitendo.

Ado ameendelea na ziara kwenye Majimbo yote ya Mkoa wa Ruvuma ambapo leo atafanya vikao katika Majimbo ya Mbinga Mjini na Nyasa.