Na George Mwigulu,Timesmajiraonline,Katavi.
VIONGOZI wa serikali wameaswa kujenga tabia ya kuwasikiliza wananchi wanapokuja na hoja za migogoro mbalimbali inayowakabili na kutafuta suluhu kwa wakati na sio kuwapuuza.
Wito huo umetolewa Julai 10, 2024 na Mwenyekiti wa Chama Cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Katavi, Joseph Mona ofisini kwake kufuatia kuwepo kwa mgogoro wa ardhi wa muda mrefu kati ya serikali ya wilaya ya Tanganyika na wananchi wa kijiji cha Luhafwe.
Mgogoro huo unahusisha eneo la Western katika kijiji cha Luhafwe linadaiwa kuwa ni eneo ambalo lipo kwenye mpango maalumu wa sehemu ya uwekezaji huku wananchi wakitakiwa kuondoka kupisha shughuli za uwekezaji zitakazofanyika humo.
Mona amesema “Wananchi zaidi ya kaya 800 wamekuwa wakiishi ndani ya eneo hilo tangu mwaka 1992 kwa bahati mbaya sana na kwa masikitiko makubwa viongozi hawako tayari kuwasikiliza licha wanahoja za msingi kuwepo katika hayo maeneo lakini leo wanaondolewa”
Mwenyekiti huyo wa ACT-Wazalendo ameweka wazi kuwa kuwapa siku 60 wananchi kupisha eneo la Western na kuwataka wahamie katika eneo la Misanga ambapo kimsingi ni eneo ambalo waliwahi kuondolewa na uharifu mbalimbali kutokea ni ajabu kuwarudisha huko na serikali inapaswa kutafakari upya.
“Kwenye suala hili la Luhafwe serikali ikae ijitafakari na wawatizame Watanzania hawa wa kaya 800 sio mchezo kuzihamisha bila utaratibu kama chama cha ACT Wazalendo tunawashauri wakae na wananchi wote na ikiwezekana wasiwabugudhi na kwa sababu Rais Dk Samia Suluhu Hassan anakuja Katavi tunaomba awasaidie” Ameeleza Mona.
Amefafanua kuwa sera za chama hicho zinauga uwekezaji nchini lakini uwekezaji unaozingatia utu wa watu kupitia kutoa elimu,kuwashirikisha wananchi na kupokea mapendekezo yao,kulinda utu wao na ikiwezekana kuwalipa fidia mambo ambayo serikali inapaswa kufuata njia hizo.
Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake wa ACT Wazalendo Mkoa wa Katavi,Anna Malaki amesema kuwa mkoa huo umebarikiwa kuwa na wanawake viongozi kwani palipo na wanawake halishindikani jambo lolote kwa sababu uongozi wa wanawake unazingatia usawa,uwajibikaji na haki.
Anna amesema kuwa utatuzi wa migogoro hususani ya ardhi hauhitaji kauli za ubabe na vitisho kwa wananchi bali unahitaji kuwajengea kwanza uelewa kupitia elimu ili watambue umuhimu wa uwekezaji na kuwapatia maeneo yaliyo bora zaidi kama mbadala wa fidia.
“Viongozi chukueni hatua kama mnaweza kuwatoa mahala ambapo wamekaa kwa miaka mingi kujitafutlia riziki basi watafutieni zuri ambalo watapa hekari hizo hizo na faida ile ile waliyokuwa wakipata na sio kuwatoa kwa nguvu bali elimu kubwa itolewe” Amesema Anna.
Mkazi wa kijiji cha Luhafwe, Paul Shija amesema kuwa hapo awali mgogoro wa maeneo kati ya wananchi na serikali ya wilaya ya Tanganyika ulikuwa na matumaini ya kutatuliwa baada ya ziara ya aliyewahi kuwa Katibu wa Itikandi na Uenezi wa Chama Chama Mapinduzi CCM, Paul Makonda lakini ghafula hapakupatikana mafanikio.
Shija ameiomba serikali kuona njia nzuri zaidi ya kutatua mgogoro huo ambao kwa muda mrefu umekuwepo na kusababisha wakati wote kuishi kwa mashaka.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato