Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
KAMATI Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo imepokea na kujadili kwa kina Ripoti ya Sekretarieti ya Chama kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na kisha kutoa maazimio,maelekezo mbalimbali ikiwemo tarehe za kuanza kuchukua na kurejesha fomu kwa wanachama wenye nia ya kuwania udiwani, ubunge na urais.
Uamuzi huo ulifikiwa na Kamati Kuu hiyo iliyokutana juzi kwenye kikao chake cha kawaida kilichofanyika jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Maalim Seif Sharif Hamad.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu ilieleza kwamba pamoja na mambo mengine, ilijadili uchukuaji na kurejesha fomu za ugombea wa udiwani, uwakilishi, ubunge na urais.
“Kamati Kuu imefungua rasmi pazia la mchakato wa uteuzi wa wagombea wa Uchaguzi Mkuu 2020. Zoezi la kuchukua, kujaza na kurejesha fomu litafanyika kuanzia Julai 1, 2020 hadi Julai 13, 2020,” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo Julai 11, mwaka huu itakuwa siku ya kikao cha Kamati Kuu na kwamba Agosti 1, 2020 itakuwa ni kikao cha Halmashauri Kuu na mchakato utahitimishwa Agosti 2, 2020 kwa Mkutano Mkuu wa Taifa wa kuwapitisha wagombea urais wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”ilieleza taarifa hiyo.
Kamati Kuu iliwataka wanachama wa chama hicho wenye nia ya kugombea kwenye nafasi za udiwani, ubunge, uwakilishi na urais wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakachukue fomu ifikapo Julai 1, 2020 hadi 13 Julai 2020.
Kupinga rushwa kwa vitendo.
Kuhusu rushwa, Kamati Kuu ilisisitiza umuhimu wa ACT Wazalendo kuendeleza utamaduni wake wa siku zote wa kupinga rushwa kwa vitendo kwa kuhakikisha kuwa vitendo vyote vya rushwa havipewi nafasi kwenye mchakato mzima wa uteuzi wa wagombea kupitia ACT Wazalendo.
“ACT Wazalendo haitamvumilia mwanachama yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa kwenye zoezi la uteuzi wa wagombea wake.
Idara ya ACT Amani imeagizwa kuchunguza na kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mgombea wa kila nafasi. Atakayebainika kushiriki vitendo vya rushwa ajue fika kuwa hana nafasi ya kuteuliwa kugombea kupitia ACT Wazalendo. Mbali na kupoteza sifa ya kuteuliwa kuwa mgombea, mwanachama atakayebainika kushiriki vitendo vya rushwa, pia atachukuliwa hatua nyingine kali za kinidhamu kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Chama,” ilieleza taarifa hiyo.
Tatu, Kamati hiyo ilieleza kwamba Mchakato wa Uchaguzi uzingatia misingi ya ACT Wazalendo.
“Kamati Kuu imewaagiza wasimamizi wote wa mchakato wa uchaguzi wa kila ngazi kuhakikisha kuwa uteuzi wa wagombea wa ACT Wazalendo unafanyika kwa kufuata misingi ya Chama, uhuru, haki, usawa na uwazi ili kusimamia demokrasia kwa vitendo kama ulivyo utamaduni wa ACT Wazalendo,” ilieleza taarifa hiyo.
Kuhusu Ushirikiano na vyama vingine makini vya Upinzani, Kamati Kuu imewapongeza viongozi wakuu wa Chama kwa jitihada wanazozifanya kuimarisha ushirikiano baina ya vyama vya upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020.
“Kamati Kuu imeridhia Chama kufanya mazungumzo ya ushirikiano na vyama makini vya upinzani ili kuingo’a CCM madarakani na kuleta mabadiliko yatakayowaletea Watanzania maendeleo,” ilieleza taarifa hiyo.
Kamati Kuu ya Chama ilisisitiza msimamo wa Chama kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2020 utakuwa wa kufa na kupona. “Chama kitahakikisha kinaulinda ushindi wake kwa mbinu zote halali na kwa gharama zozote,” ilieleza taarifa hiyo.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito