December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Achangia milioni 1,shule ya sekondari kamsamba

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online Songwe

MDAU wa maendeleo mkoani Songwe Ombeni Nanyaro ametoa kiasi cha milioni 1 ,kwa ajili ya kuvuta maji ya kukarabati bweni la wanafunzi wa shule ya sekondari Kamsamba wilayani Momba mkoani Songwe.

Nanyaro ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya shule hiyo na Mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM Mkoa ametoa kiasi hicho cha fedha baada ya kufanya ziara ya kuitembelea shule hiyo inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuona wanafunzi wakitembea kilometa 3 hadi mtoni kusaka maji ambayo si safi na salama.

Akizungumza mara baada ya kutoa fedha hizo amesema baada ya kuona adha hiyo inaowakabili wanafunzi wa shule hiyo aliamua kuwaita mafundi kuvuta maji na kutoa mifuko ya saruji na mchanga kwa ajili ya ukarabati wa bweni.

Nanyaro amesema tayari ameunganisha maji safi na wanafunzi wameanza kuyatumia huku mpango uliopo ni kununua vitanda na magodoro ikiwemo kulikarabati bweni la wanafunzi kwani limechoka na halina hadhi kutumiwa.

“Nilio ahidi nitayakamilisha hivi punde,nikimaliza nitaweka ‘compyuter’ madaras ani na tv kwenye mabweni ili wanafunzi wajisikie wapo nyumbani”amesema.

Suma Mwashitete mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo amesema wataepukana na vihatarishi hata vya kufanyiwa ukatili pindi waendapo kuchota maji mtoni na kuwa ukarabati wa bweni utawapa hamasa ya kusoma.