November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ACC yawanoa wadau kuhusu Malezi ,Makuzi ya watoto

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WADAU mbalimbali wakiwemo viongozi kutoka Idara za Serikali,Mpango wa Kudhibiti Ukatili dhidi ya wanawake na Watoto (MTAKUWWA),Madiwani na viongozi wamepatiwa elimu juu ya utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) inayotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano.

Akizungumza katika warsha hiyo,Afisa Maendeleo kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Salome Fransis amesema,jamii nzima inapaswa kuelewa kuhusu programu hiyo iweze kuitekeleza Programu hiyo ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwake ambayo ni kuhakikisha mtoto anafikia ukuaji timilifu na kuleta tija katika Taifa.

Aidha amesema Programu hiyo imeanzishwa baada ya kuona kuna baadhi ya changamoto ambazo hazijatekelezwa katika sera na miongozo mbalimbali inayomuhusu mtoto huku akisema mipango na programu nyingi za watoto zimelenga umri wa miaka 0-5.

“Sasa Programu hii ya MMMAM inaangalia watoto wenye umri kuanzia miaka  0-8,ili kuwekeza kwa kundi la watoto wenye umri huo katika kuhakikisha mtoto anapata afya bora,lishe ya kutosha,ujifunzaji elimu ya awali,ulinzi na usalama pamoja na malezi yenye mwitikio.”amesema Salome na kuongeza kuwa

“Kwa mfano ,suala la malezi yenye mwitikio halipo kabisa kwenye sera na miongozo mbalimbali iliyotangulia ,lakini kimsingi mzazi napaswa kuitikia mahitaji ya mtoto ,hii humwezesha kukua vyema.”

Kwa upande wake Afisa kutoka Mtandao wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (TECDEN) Christopher Peter amesema,katika kipindi cha umri wa miaka 0-8 ndio wakati ambao ubongo wa mtoto unatengenezwa ,hivyo mtoto anapaswa kulelewa kwa kuzingatia maeneo muhimu ya afya,lishe,ujifunzaji wa awali,ulinzi na usalama pamoja na malezi yenye mwitikio ili ajifunze vyema na kufikia ukuaji timilifu.

Aidha amesema,vitu vya muhimu katika makuzi ya ubongo wa mtoto ni pamoja na kuhakikisha mtoto anapata lishe ya kutosha,anacheza,anapata maji safi na salama na apumzike vya kutosha huku akisema,mtoto anazaliwa huku ubongo wake ukiwa na asilimia 25 na asilimia zinazobaki zinategemea sana malezi kutoka kwa wazazi na jamii inayomzunguka kwa ujumla.

“Hata mtu akitaka kujenga ni lazima anaanza kuimarisha msingi ili kuiimarisha nyumba yake,na ndivyo tunavyotakiwa kuweka msingi mzuri kwa watoto wetu kuanzia wakiwa tumbani (kipindi cha ujauzito) hadi anapofikisha miaka minane kwa sababu hiki ndicho kipindi ambacho ubongo wa mtoto hukua kwa kasi lakini pia hushika vitu kwa urahisi.”amesema Christopher

Kwa upande wa washiriki wamafunzo hayo wamesema kama PJT-MMMAM itazingatiwa katika utekelezaji wake itasaidia Taifa kupata watu wenye weledi na hivyo kuleta tija ya kutosha zaidi hapo baadaye.

Diwani wa Kata ya Bahi Mjini Augustino Ndonu ameahidi kupeleka mafunzo hayo kwa wananchi wake kwa kutumia vikao mbalimbali vikiwemo vya maendeleo ya Kata hiyo kwa kushirikiana na Afisa Ustawi wa Halmashauri ya Bahi .

“Programu hii inaonyesha kuna mahali kama wazazi tumefeli,maana unakuta kuna mzazi mwingine anampeleka mtoto shule na anapomkabidhi kwa mwalimu anamwambia mtoto huyu amenishinda ,sasa amekushindaje wakati wewe ndiyo mwalimu wa kwanza ,hii inaonyesha kuna mahali kama wazazi tunafeli na tunahitaji kurekebisha katika eneo la malezi ya watoto wetu.”amesema Ndonu

Naye Padre Nazary Njiku kutoka wilaya ya Kondoa amesema,Programu hii ya Malezi na Makuzi ya Mtoto ni fursa kwa jamii kuwalea watoto na kuwafanya wawe wanajamii bora.

Siku kwa siku kumekuwa na matukio ya unyanyasaji wa watoto yanazidi kuongezeka hivyo kupitia programu hii tunaona kuna kila namna ya kufikisha elimu kwa wazazi ili waweze kuwalea watoto mazingira mazuri licha ya kuwa wanapita katika changamoto nyingi zikiwemo za utandawazi.

Mjumbe wa Kamati ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) wilaya ya Chamwino Joanita Kahangwa amesema katika mazingira yaliyopo watoto wanapata changamoto katika makuzi yao,wanabakwa na kulawitiwa hii ni kutokana na wazazi wengi kupambana na harakati za maisha .

“Wazazi wengi hususan wakina mama,tumeacha kukaa na watoto ,muda miwngi hatuwasikilizi,unakuta mtoto anakuja na shida yake mama anamfukuza na kumtaka akacheze ,kwa hiyo kupitia mafunzo haya tumeona umuhimu wa wazazi kukaa na watoto na kuwasikiliza mahitaji yao.”amesema Joanita

Aidha ameiomba Serikali kuangalia upya walimu wa madarasa ya awali kwani uzoefu unaonyesha madarasa mengi ya awali hayana walimu wenye elimu ya awali.

Warsha hiyo imeandaliwa na shirika lisilo la Kiserikali la Action for Community Care linalotekeleza mradi wa Mtoto kwanza mkoani Dodoma unaochochea utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Kitaifa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto  kwa ufadhili wa Mtandao wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (TECDEN) .