Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC)limesema hadi sasa jumla ya abiria waliosafirishwa na reli ya SGR ni takribani milioni 2.1 na kiasi cha shilingi bilioni 59 zimekusanywa kama mapato.
Hiyo ni toka kuanza kwa uendeshaji wa reli ya SGR kati ya Dar es salaam hadi Dodoma mnamo Juni 14,2024 na Dar es salaam hadi Morogoro Julai 25,2024.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Machi 22,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa TRC,Masanja Kadogosa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu sita.
Kadogosa amesema mafanikio ya uendeshaji wa Reli ya SGR ni kupatikana kwa usafiri na usafirishaji wenye staha na gharama nafuu,upunguza muda wa safari, uendeshaji wa reli ya SGR bila ruzuku ya Serikali, kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi na upatikanaji wa ajira ambapo ajira zaidi ya 30,176 za moja kwa moja na ajira zaidi ya 150,880 zisizo za moja kwa moja zimezalishwa kupitia miradi hiyo.
Ametaja mafanikio mengine kuwa utunzaji wa mazingira ambapo takribani tani 14,327.3 za hewa ya ukaa zimepungua, kusafirisha mzigo mkubwa kwa mara moja ambapo treni moja itabeba kiasi cha tani 3,000 kwa wakati mmoja, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, kupungua kwa gharama za matengenezo ya barabara kutokana na mzigo mkubwa kusafirishwa kwa njia ya reli, kuchangia ufanisi wa bandari na ukuaji wa sekta zingine pamoja na kuchagiza ukuaji wa miji katika maeneo yaliyopo katika ushoroba wa reli.
“Sekta ya uchukuzi hususan kwa njia ya reli ni moja ya kichocheo cha kukuza uchumi na ni chanzo cha kuongeza mapato ya Taifa kwa njia moja au nyingine. Kwa namna ya pekee tunaishukuru na kuiomba Serikali iendelee kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji ili kuchagiza ukuaji wa uchumi wa nchi,”amesema Kadogosa.
Aidha Mkurugenzi huyo amesema uendeshaji wa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma umeendelea kwa ufanisi mkubwa na Shirika kupitia maelekezo mbalimbali ya viongozi limeendelea kuboresha utoaji wa huduma ya kusafirisha abiria kwa kutumia reli ya SGR ili kuhakikisha usafiri kwa njia hiyo unakuwa salama na wa uhakika na kuchochea uzalishaji mali.
Vilevile Kadogosa amesema kuwa huduma za usafirishaji wa mizigo inatarajia kuanza mwezi Aprili 2025 kufuatia kukamilika kwa majaribio ya mabehewa 264 ya mizigo yaliyowasili nchini Disemba 2024.
Hata hivyo Kadogosa amesema pamoja na utekezaji wa miradi ya SGR, shirika limeendelea na utekelezaji ya miradi kwa ajili ya kuboresha reli ya kati ya MGR, ikiwemo ukarabati wa Reli ya Kati ya Dar es Salaam – Isaka (Awamu ya Kwanza), ukarabati wa njia ya reli hadi uwezo wa ratili 80.
“Miradi mingine ni ukarabati wa Reli ya Kaliua – Mpanda (210KM), ambapo kazi zinazofanyika ni pamoja na kuboresha njia kwa kutumia reli za ratili 80, pamoja na ukarabati wa madaraja,”amesema.
Vile vile amesema TRC inatekeleza ujenzi wa Daraja na Mabadiliko ya Njia Kati ya Godegode na Gulwe, ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 175 katika km 349+450 (Kati ya Stesheni ya Godegode na Gulwe) na urekebishaji wa njia kwa urefu wa km 6.2.



More Stories
Kakulima:Lushoto ni eneo muhimu kwa shughuli za utalii
Viongozi CHADEMA, Odinga wakutana, wajadili hali ya kisiasa nchini
Kamati ya Bunge yaridhishwa na ujenzi wa miradi kupitia mapato ya ndani