January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aachana na kufanya vibarua, atumia ruzuku kuanzissha kilimo cha nyanya

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Chato

MNUFAIKA wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ameanzisha kilimo cha nyanya, ambacho anatarajia kitakuwa mkombozi kwenye maisha yake.

Mnufaika huyo, Bi. Joyce Kishutungu Shikimai (44) mkazi wa Kibilizi C, wilayani Chato, mkoani Geita, anasema ameanzisha kilimo hicho baada ya kupata ruzuku kutoka kwenye mfuko huo.

Mbali na kuanzisha kilimo hicho, Bi. Joyce anasema ana mgahawa wa wa kuuza uji ambao nao aliuanzisha kwa fedha za TASAF.

“Kwa hiyo faida ninayopata kwenye uji niliichanganya na fedha za TASAF, nikakodi shamba, nikaweka watu wa kunilimia nikaanza kilimo cha nyanya,” anasema Bi. Joyce na kuongeza;

“Sasa hivi naendelea kuhudumia shamba langu, nikipata faida kwenye uji nanunua dawa na kwa hali inavyokwenda nina matumaini kilimo hiki kitabadili maisha yangu.”

Aidha, anasema amejiunga kwenye kikundi cha Umoja ni Nguvu, ambacho kinaundwa na wanawake wanufaika wa TASAF, ambapo kila wiki mwanakikundi ananunua hisa kuanzia sh. 1,000 na fedha za jamii ni 1,000.

Anasema ndani ya kikundi hicho wamekuwa wakikopeshana. “Kwa hiyo nikichukua mkopo kwenye kikundi na kwenye biashara ,nanunua dawa, kwa ajili ya kunyunyizia shamba la nyanya na nikipata faida kwenye biashara ya uji narudisha mkopo kwenye kikundi,” anasema.

Kwa mujibu wa Bi. Joyce kama isingekuwa TASAF asingeweza kuanzisha mradi wa uji, wala kilimo cha nyanya.

Kabla ya kujiunga na TASAF, Bi. Joyce anasema alikuwa na hali ngumu ya maisha, kwani ana mtoto mmoja wa kumzaa na baada ya wazazi wake kufariki, aliachiwa jukumu la kulea wadogo wake saba, hivyo wakawa jumla nane.

“Ilikuwa ni vigumu sana kuwapatia mahitaji ya shule na mengine, kula kulikuwa kwa shida. Nilitegemea kufanya vibarua, ambavyo navyo havikutosheleza mahitaji ya familia,” anasema Bi. Joyce.

Anasema mgahawa wa uji ulimsaidia kusomesha watoto hadi wakahitimu darasa la saba, ambapo baadhi yao tayari wameanza kujitegemea na kwamba kadri mzigo wa kulea watoto unavyopungua, ndivyo anavyobuni shughuli nyingine ya kufanya, kama alivyoanzisha kilimo cha nyanya.