December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

watumishi Ilemela waelimishwa juu ya kujikinga na ugonjwa wa marburg

Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Kufuatia uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa marburg,Mkoa wa Kagera,watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza,wamepatiwa elimu ya namna ya kujikinga na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Elimu hiyo imetolewa na idara ya afya ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ikiongozwa na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt.Samson Marwa.

Akizungumza wakati akitoa elimu hiyo Mganga Mfawidhi hospitali ya Wilaya ya Ilemela Dkt.Mateso Mayunga ameeleza kuwa ugonjwa wa marburg ni moja ya magonjwa machache lakini ni hatari sana.

Ugonjwa huo unaosababisha hali ya kuvuja damu sehemu za wazi ambao huathiri zaidi binadamu pamoja na wanyama jamii ya nyani.

Dkt.Mayunga amesema ugonjwa huu husambaa kupitia kugusa majimaji ya mtu mwenye ugonjwa ,marehemu aliefariki kwa ugonjwa huo au kugusa kitu chenye virusi hao.

Huku akisisitiza kuwa kwa sasa jamii inapaswa kupunguza kugusana hasa kwa kushikana mikono wakati wa kusalimiana.

Pamoja na kuboresha tamaduni za usafi kwa kunawa mikono mara kwa mara,kuepuka kushiriki mazishi ya kimila kwa marehemu aliyefariki kwa ugonjwa au kifo tatanishi,kuepuke kula nyama pori au kugusa mizoga ya wanyama pori kama vile popo na nyani.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt.Samson Marwa amezitaja dalili za ugonjwa huo ambazo hutokea ghafla ni pamoja na homa ,baridi,maumivu ya kichwa ,maumivu ya misuli na wakati mwingine mgonjwa kutokwa na upele mkubwa mwilini hasa maeneo ya kifuani,mgongoni au tumboni.

Hivyo waepuke misongamano isiyokuwa ya lazima na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanapo ona dalili au mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.

“Ni wajibu wetu kujikinga zaidi kwani mpaka sasa ugonjwa huu hauna tiba maalum,hapa kwetu ugonjwa bado haujafika ni lazima tuchukue tahadhari,”ameeleza Dkt.Marwa.

Naye mmoja wa watumishi katika Halmashauri Manispaa ya Ilemela Beater Boniface, ameeleza kuwa wao watumishi ni mabalozi wazuri kwa watu wengine huko mtaani na nyumbani sababu wamepewa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa marburg.

Hivyo ameishukuru idara ya afya kwa kuona umuhimu wa watumishi kuelewa hilo kwa wakati.

Kwa mara ya kwanza Tanzania ilitangaza uwepo wa ugonjwa huo Machi 21, 2023 katika Mkoa wa Kagera wilayani Bukoba.Mpaka sasa watu wanane (8) wamepata maambukizi na kati yao watano (5) walifariki na watatu (3) wanaendelea na matibabu.