March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

 DCEA yateketeza dawa za kulevya jijini Dar-es-Salaam 

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA),  imeteketeza jumla ya kilogramu 4,402.02 za dawa za kulevya katika kiwanda cha saruji cha Twiga, kilichopo Wazo, jijini Dar-es-Salaam.

Kati ya hizo kilogramu 2,168.18 ni dawa za kulevya aina ya methamphetamine, kilogramu 1,064.29 za heroin, gramu 326.95 za cocaine, kilogramu 515.48 za bangi na kilogramu 653.74 za mirungi.

Dawa hizo ambazo zimeteketezwa zilikuwa zikihifadhiwa kama vielelezo vya mashauri mbalimbali ya kesi zinazohusu dawa za kulevya.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini humo,Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, inayotaka vielelezo vya aina hiyo kuharibiwa wakati kesi ikiendelea au baada ya hukumu kutolewa.

“Mahakama iliagiza dawa hizo ziteketezwe kutokana na hatari ya kuharibika au kubadilika umbo kama Sheria inavyotaka,”amesema Lyimo.

Miongoni mwa dawa za kulevya zilizoteketezwa huku mashauri yakiendelea makahamani ni kesi ya Najim Abdallah Mohamed, iliyohusisha dawa za kulevya aina ya heroin kilogramu 882.71 na dawa ya kulevya aina ya methamphetamine kiasi cha kilogramu 2,167.29. 

 Aidha, dawa za kulevya zilizoteketezwa wakati mashauri yanayohusiana na dawa hizo yalishatolewa hukumu na washitakiwa walipatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo ni pamoja na kesi ya  Hassan Azizi, Salum Shaaban Mpangula na Hemed Juma Mrisho maarufu kwa jina la “Hororo”, waliohukumiwa kifungo cha maisha jela.

Huku Gumbo Ramadhani Ally,akihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, Irene Dickson Mseluka kifungo cha miaka mitano jela na Gema Victor Mmasy kifungo cha miaka mitatu jela.

Vilevile Kamishna Jenerali  Lyimo aliwaonya wanaofanya biashara ya dawa za kulevya kuacha mara moja kwani mamlaka haitawafumbia macho. 

“Mamlaka itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kisheria na kiutendaji ili kuhakikisha Tanzania inalindwa dhidi ya athari za dawa za kulevya,” amesema Lyimo.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kupiga vita dawa za kulevya huku ikisisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa hizo ni jukumu la kila mmoja.