Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
WATU wenye changamoto ya kutoona kutoka mikoa ya Dar-es-Salaam na Pwani wamenufaika na mafunzo yaliyotolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa lengo la kuwawezesha kushiriki shughuli za uzalishaji kwa kuzingatia kanuni bora za usalama na afya kazini.
Mafunzo hayo ya siku moja ambayo yametolewa kwa wanachama 50 wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania ( TAB) yamehusisha mada mbalimbali zikiwemo utambuzi na udhibiti wa vihatarishi vya usalama na afya pamoja na misingi ya huduma ya kwanza mahali pa kazi.

Ambao wanajihusisha na shughuli mbalimbali zikiwemo ushonaji, kilimo, ufugaji, uzalishaji wa bidhaa zikiwemo sabuni na biashara ndogo ndogo.
Akifungua mafunzo hayo Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema taasisi inatambua thamani na mchango wa watu wenye ulemavu katika kujenga uchumi wa taifa.
“Nidhahiri kuwa ulemavu ni hali tu ambayo hazipaswi kuwa kikwazo kwenu kushiriki katika shughuli za kiuchumi,tunawapatia vifaa saidizi zikiwemo fimbo nyeupe, karatasi za nukta nundu pamoja na vitabu maalumu vya nukta nundu vyenye maudhui ya mafunzo ya usalama na afya kwa ajili ya rejea zaidi,”amesema Mwenda.
Mwenda ameahidi kuwa mafunzo ya usalama na afya kwa makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu yatafuatiwa na zoezi la kutembelea maeneo yao ya kazi kwa ajili ya kutathmini mazingira ya kazi, ili kushauri namna sahihi ya kuboresha mazingira hayo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania,Omary Itambu, ameipongeza OSHA kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha watu wasioona pamoja na makundi mengine ya watu wenye ulemavu.
“Niwahakikishie OSHA kuwa mafunzo mliotupatia si tu yatakwenda kuimarisha afya na usalama wetu,bali yatatusaidia sana kuongeza thamani ya huduma ya bidhaa tunazozalisha,” amesema Itambu.
Naye Mratibu wa Idara ya Vijana wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania,Bakari Hassani amesisitiza kuwa mafunzo hayo na vifaa saidizi walivyopewa vitarahisisha utendaji na kuongeza tija katika shughuli zao za kila siku.

.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi